Mvua kubwa na mafuriko yamesababisha vifo vya takriban watu 58, wakiwemo watoto, nchini Tanzania tangu mwanzoni mwa Aprili.
Kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi, ukanda wa Pwani ndio ulioathirika zaidi ambapo watu 33 kati ya 58 wamefariki katika mkoa wa Morogoro na Pwani.
“Kuanzia Aprili 1 hadi Aprili 14, 2024, kulikuwa na vifo 58 vilivyosababishwa na mvua kubwa, ambayo ilisababisha mafuriko,” Mobhare Matinyi aliuambia mkutano na waandishi wa habari, akisisitiza kuwa ukanda wa pwani wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ni mojawapo ya walioathirika zaidi.
Aprili ni kilele cha msimu wa mvua nchini Tanzania.
“Madhara makubwa ya mafuriko yanashuhudiwa katika eneo la pwani ambapo watu 11 hadi sasa wamefariki,” aliongeza.
Siku ya Ijumaa, watoto wanane wa shule walifariki baada ya basi lao kutumbukia kwenye korongo lililofurika mkoani Arusha.
Mtu aliyejitolea katika shughuli za uokoaji pia alifariki.
Zaidi ya kaya 10,000 zimeathirika na zaidi ya mashamba 75,000 yameharibiwa na mafuriko katika maeneo ya pwani na Morogoro — yaliyoko kilomita 200 (maili 124) magharibi mwa mji mkuu wa kiuchumi Dar es Salaam.
Mvua za msimu wa mwaka huu zimechangiwa na hali ya hewa ya El Nino, wataalamu wa hali ya hewa wameonya.
El Nino inayotokea kiasili, ambayo iliibuka katikati ya mwaka wa 2023, kwa kawaida huongeza viwango vya joto duniani kwa mwaka mmoja baadaye.
Pia inaweza kusababisha ukame katika sehemu fulani za dunia na mvua kubwa katika maeneo mengine.
Wanasayansi kutoka kundi la World Weather Attribution wamesema mvua katika Afrika Mashariki “ilikuwa mojawapo ya mvua kubwa kuwahi kurekodiwa” katika eneo hilo kati ya Oktoba na Desemba.
“Mabadiliko ya hali ya hewa pia yalichangia tukio hilo, na kufanya mvua kubwa kunyesha hadi mara mbili zaidi,” walisema, na kuongeza kuwa mchango kamili wa ongezeko la joto haujulikani.