Watu nane wafariki kwenye ajali iliyohusisha Lori na magari mengine mawili

Watu nane wamefariki dunia na wengine ambao idadi yao haijafahamika wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea leo Jumanne, Agosti 16, 2022 eneo la Shamwengo karibu na kituo cha mafuta Inyala mkoani Mbeya.

 Kamanda wa jeshi la Polisi mkoani humo, Urlich Matei amethibitisha kutokea tukio hilo akisema gari kubwa lililokuwa limebeba kontena la mchanga lilifeli breki na kuligonga basi la Super Rojas lililokuwa likitoka Mbeya kwenda Njombe.

Amesema baada ya kugonga basi hilo, liliendelea kushuka zaidi na kuligonga gari lingine lenye aina ya benzi na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa ambao idadi yao haijajulikana haraka.

Waliopoteza maisha ni nane japokuwa bado idadi rasmi haijajulikana ila baadaye taarifa ya daktari itaeleza kwa ujumla, ila majeruhi wamesambazwa kwenye hospitali tofauti ikiwamo Igawilo na Mkoa,” amesema Matei.

Kamanda huyo amesema chanzo kikubwa katika ajali hiyo ni kufeli breki kwa gari hilo na kubainisha barabara hiyo ni finyu na kwamba tayari wameanzisha ukaguzi wa maroli yanayotumia njia hiyo.