Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limekamata watu saba wanaotuhumiwa kumuua hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Joackim Mwakyolo (51).
Katika tukio hilo, mtu mwingine ambaye jina lake halijafahamika, aliuawa baada ya kushambuliwa kwa mawe na kuwakata na vitu vyenye ncha kali kichwani na miguuni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga alisema jana kuwa mauaji hayo yalitokea Januari 20 mwaka huu katika Kijiji cha Kibole wilayani Rungwe mkoani humo.
Kamanda Kuzaga alisema chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa ardhi baina ya Mwakyolo na kijiji hicho.
Alisema hakimu huyo alikuwa akishitakiana na kijiji hicho kuhusu ardhi inayokadiriwa kuwa na ekari 600 kwa kuwa serikali ya kijiji inadai kuwa ni hifadhi ya msitu wa kijiji hicho lakini yeye alidai alinunua eneo hilo kwa wenyeji.
Kuzaga alisema mgogoro huo ulifika ngazi ya Mahakama Kuu kupitia shauri la ardhi namba 08/2018 Joachim Mwakyolo dhidi ya Halmashauri ya Kijiji cha Kibole na wanakijiji 22 katika mahakama kuu Kanda ya Mbeya.
Mwakyolo aliishitaki serikali ya kijiji na baadhi ya wananchi wa kijiji hicho kuwa wameingia kwenye eneo lake na shauri hilo liliisha Desemba 2021 kwa serikali ya kijiji na wanakijiji kupata ushindi.
Kamanda Kuzaga alisema Januari 20 saa 2:00 usiku, hakimu huyo na wenzake wawili walionekana wakitoka katika eneo la mgogoro ndipo baadhi ya wananchi waliokuwa kilabuni walimvamia na kuanza kumhoji.
Alisema ulizuka ugomvi kati yao na Mwakyolo alikuwa na silaha, pistol aliyoifyatua risasi na kuwajeruhi watu wawili ambao ni Tubuke Kisasa (48) na Huruma Mwamakigula (45) kabla ya kundi la wananchi kuwashambulia na kuwaua.
Aliwataja watuhumiwa wa mauaji hayo ni Ambokile Mwakagundya (30), Zawadi Mwakagile (27), Lutengano Mwakagile (27), Wito Mwakatobe (19), Lwitiko Kikomile(27), Aliko Mwakikyo (40),Tubuke Kisasa (48) wote wakiwa ni wakazi wa Kijiji cha Kibole.
Mmoja wa majeruhi wa risasi hiyo, Mwamakigula alidai kuwa alisikia mzozo wa watu na baadaye alimsikia mumewe akilia kuwa amepigwa risasi na aliposogelea eneo la tukio nae alipigwa risasi mguuni.