Watu wenye silaha wamewateka nyara watawa wanne wa Kikatoliki katika jimbo la Imo kusini-mashariki mwa Nigeria, katika ghasia za hivi punde katika eneo ambalo mivutano ya wanaotaka kujitenga inazidi kuongezeka.
Utekaji nyara unaofanywa na magenge ya wahalifu hutokea mara kwa mara katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika, lakini katika wiki za hivi karibuni waumini wa makanisa ya Kikristo wamezidi kulengwa.
Mateka wengi huachiliwa baada ya malipo ya fidia, lakini wengine wameuawa.
“Madada wanne wa kanisa katoliki walitekwa nyara,” msemaji wa polisi wa jimbo la Imo Michael Abattam aliambia AFP.
Alisema watawa hao walikamatwa karibu na jiji la Okigwe siku ya Jumapili wakielekea kwenye misa.
“Tuko katika msururu wa watekaji nyara kwa nia ya kuwaachilia waathiriwa,” alisema.
Abattam hakuweza kueleza mara moja sababu za utekaji nyara huo kwani hakuna kundi lililodai kuhusika.
Kusini-mashariki mwa Nigeria kumeshuhudiwa kuongezeka kwa ghasia zinazolaumiwa kwa kundi lililopigwa marufuku la Watu wa Asili wa Biafra (IPOB) au tawi lake linalojihami la ESN.
IPOB ambayo inatafuta jimbo tofauti kwa ajili ya watu wa kabila la Igbo imekanusha mara kwa mara kuhusika na vurugu katika eneo hilo.
Zaidi ya maafisa wa polisi 100 na maafisa wengine wa usalama wameuawa tangu mwanzoni mwa mwaka jana katika mashambulizi yaliyolengwa katika eneo hilo, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
Magereza pia yamevamiwa na wafungwa wengi kuachiliwa na kuibiwa silaha.
Kiongozi wa IPOB Nnamdi Kanu yuko chini ya ulinzi wa serikali tangu wakati huo na anakabiliwa na kesi ya uhaini.
Utengano ni suala nyeti nchini Nigeria ambapo kutangazwa kwa Jamhuri huru ya Biafra mwaka 1967 na maafisa wa jeshi la Igbo kuliibua vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya zaidi ya watu milioni moja.