Watu zaidi ya 20 wameripotiwa kufariki dunia nchini Sudan, kufuatia mvua kubwa ambayo imesabab isha maporomoko ya majengo.
Maafa hayo yanajiri wakati nchi hiyo ikikabiliwa na takriban miezi 16 ya mapigano kati ya vikosi hasimu vya usalama, daktari aliiambia AFP Jumanne.
“Watu tisa wamekufa kutokana na nyumba zao kuporomoka,” alisema mfanyakazi katika hospitali ya Abu Hamad, mji mdogo katika jimbo la Nile nchini Sudan, baadhi ya kilomita 400 (karibu maili 250) kaskazini mwa Khartoum
“Watu wengi waliojeruhiwa wanaendelea kuwasili hospitalini”, chanzo hicho kiliongeza.
Kila mwaka mwezi wa Agosti, mvua kubwa ambao hushuhudiwa husabisha mto Nile kuvunja kingo zake kutokana maji mengi ambayo huishia kusababisha uharibifu mkubwa katika makazi ya binadamu, miundombinu na hata watu kupoteza maisha kutokana na maradhi ya kipindupindu na magonjwa mengine yanayotokana na maji.
Athari hiyo inatarajiwa kuwa mbaya zaidi mwaka huu baada ya mapigano ya zaidi ya mwaka mmoja ambayo yamesukuma mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao katika maeneo ya mafuriko.
“Mvua kubwa ilisababisha nyumba nyingi kuanguka na maduka yote sokoni kuanguka,” shahidi katika Abu Hamad aliambia AFP kwa njia ya simu.
Wiki iliyopita, mafuriko makubwa yalisababisha vifo vya watu watano huko Port Sudan, kwenye ufuo wa Bahari Nyekundu.
Mashirika ya misaada yameonya mara kwa mara kwamba juhudi zao za kutoa msaada wa kibinadamu, ambao tayari umetatizwa na vita, unahofiwa kulemazwa katika baadhi ya maeneo wakati msimu wa mvua unapoingia.
Sudan inakabiliwa na kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani katika kumbukumbu za hivi karibuni, kwani mapigano kati ya jeshi na vikosi vya kijeshi vya Rapid Support Forces hayaonyeshi dalili ya mapigano hayo kupungua.
Baadhi ya watu milioni 10.5 wamelazimishwa kutoroka makwao, janga la njaa likitarajiwa kuvamia chi hiyo.