Watuhimiwa kufanya utekaji na kuwabaka warembo

Prisoner

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linawashikiria watu wawili wanaodaiwa ni viongozi wa mtandao wa utekaji, uporaji na ubakaji wanawake maarufu na warembo katika Jiji la Arusha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jastin Masejo amethibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuongeza kuwa kuna watuhumiwa zaidi wamekamatwa wakidaiwa kushirikiana na mtandao huo.

Taarifa zinadai kuwa watuhumiwa wa awali walikamatwa usiku wa Aprili 21, mwaka huu.

Kamanda Masejo alisema  kuwa, polisi wanawatafuta waliohusika kwa namna moja ama nyingine kwenye matukio hayo ili wajibu mashitaka.

Alisema kwa sasa ni mapema kutaja majina ya watuhumiwa  kwani inaweza kuharibu ushahidi kwa kuwa watuhumiwa wengine bado wanatafutwa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha zilidai kuwa watuhumiwa hao walikuwa wakitumia gari ndogo kuteka wanawake kwa kuwafunga vitambaa usoni, kuwapeleka wanakotaka, kuwabaka, kuwapora fedha na mali na kuwatupa na kutokomea.

Vyanzo vya habari vilidai wanawake waliofanyiwa vitendo hivyo wametoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha kesi zaidi ya 20 wakidai kufanyiwa unyama huo.

Inadaiwa watuhumiwa hao huwafuata walengwa katika klabu za starehe au hoteli kubwa na hutongozwa na baadhi ya viongozi wa mtandao huo na kisha kufanyiwa unyama huo.

Taarifa zilidai baada ya watuhumiwa hao kukamatwa walipekuliwa majumbani mwao na kukutwa na vitu vya thamani zikiwamo cheni za dhahabu, hereni za dhahabu, saa za aina mbalimbali na simu za mkononi.

”Watuhumiwa wamekiri kuhusika katika utekaji, uporaji na ubakaji wanawake na wametoa ushirikiano kwa polisi kwa kueleza mtandao wote na wengine wanasakwa kwa uhalifu huo,” alisema mtoa taarifa ndani ya Jeshi la Polisi Arusha.

CHANZO Habari Leo.