Watuhumiwa wa mauaji ya askari Ngorongoro waachiwa huru

Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imewaachia huru washitakiwa 24 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya mauaji ya askari polisi wilayani Ngorongoro baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha nia ya kutoendelea na kesi hiyo.

Kesi hiyo ambayo leo Jumanne, Novemba 22, 2022 ilipangwa kwa ajili ya kutajwa ambapo kati ya washitakiwa hao 24, kumi ni madiwani pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Ngorongoro, Nderango Laizer.

Mbele ya Hakimu Mkazi Herieth Mhenga, Jamhuri katika kesi hiyo ya mauaji namba 9/2022 iliwakilishwa na wakili Upendo Shemkole ambaye aliieleza mahakama shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

Aidha, aliieleza mahakama DPP kwa niaba ya Jamhuri hana nia ya kuendelea kuwashitaki watuhumiwa hao na kuomba kuondoa shauri hilo mahakamani kifungu 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa makosa ya jinai.

Baada ya ombi hilo, Hakimu alisema mahakama haina budi kuridhia maombi hayo na kesi hiyo kuondolewa na washitakiwa wote 24 kuachiwa huru.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Molongo Paschal, Albert Selembo, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Ingoi Olkedenyi Kanjwel, Sangau Morongeti, Morijoi Parmati, Morongeti Meeki, Kambatai Lulu, Moloimet Yohana na Joel Clemes Lessonu.

Wengine ni Simon Orosikiria, Damian Rago Laiza, Mathew Eliakimu, Luka Kursas, Taleng’o Leshoko, Kijoolu Kakeya, Shengena Killel, Kelvin Shaso Nairoti, Wilson  Kiling, James Taki, Simon Saitoti na Joseph Lukumay.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa mawili ambapo kosa la kwanza ni njama ya mauaji, ambapo wanadaiwa kupanga njama ya kuua maafisa wa serikali na maafisa polisi watakaoshiriki zoezi la kuweka mipaka pori tengefu la Loliondo.

Kosa la pili ni mauaji ambapo wanadaiwa Juni 10, 2022 eneo la Ololosokwan, wilayani Ngorongoro kwa nia ovu walisababisha kifo G 4200 Koplo Garlus Mwita.

Hadi wanaachiwa huru hii leo wamekaa mahabusu kwa muda wa zaidi ya miezi mitatu.