Wavuvi watatu wahofiwa kufariki Ziwa Victoria

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibushubwamu

Watu watatu wanahofiwa kufariki dunia huku mmoja akinusurika baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kuvua samaki kupigwa na dhoruba na kisha kuzama.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibushubwamu amesema kuwa tukio hilo lilitokea Ijumaa iliyopita ndani ya ziwa Victoria katika kisiwa cha Rukuba wilayani Musoma.

Kamanda Tibushubwamu amesema kuwa siku hiyo wavuvi wanne waliingia ziwani usiku kuvua dagaa lakini wakiwa wanaendelea na shughuli zao ghafla yaliibuka mawimbi makubwa ziwani na kupelekea mtumbwi wao kupigwa na dhoruba na kupasuka kisha kuzama majini.

Amewataja watu wanaohofiwa kufariki dunia kuwa ni pamoja na Kaida Mafuru (37), Frank Magwinya 35 na mtu mwingine anayetambulika kwa jina moja la Jeti (30).

Amesema kuwa aliyenusurika ni Peter Willim (35) baada ya kufanikiwa kushika ubao uliopasuka kutoka mwenye mtumbwi hivyo kuelea ziwani hadi asubuhi alipookolewa na amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Mara akiendelea na matibabu.

“Hawa watu watatu hatuna uhakika kama wamefariki au la kwasababu hadi sasa bado hawajapatikana tangu tukio lilivyotokea lakini oparesheni inaendelea ziwani kuwatafutwa aidha wawe wamekufa au wako hai na hivi tunavyoongea boti kadhaa zipo eneo la tukio zikiendelea kuwatafuta” amesema Kamanda Tibushubwamu