Mwanzo Tv

Nairobi Kenya

+254 7

24/7 Customer Support

Mon - Fri: 9:00 - 17:30

Online Media always open

Waziri aingilia kati sakata la kupanda kwa bei za vinywaji na vifaa vya ujenzi

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji ametoa siku tatu kwa Tume ya Ushindani nchini (FCC) kumpatia taarifa ya sababu ya vinywaji baridi kuadimika sokoni na bei yake kupanda.

Aidha, Dk Kijaji pia ametoa siku saba kwa tume hiyo kufanya utafiti na kumpatia taarifa zilizosababisha kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji, mabati pamoja na nondo.

Amesema bidhaa zote hizo zina ushindani sokoni na haelewi  kwanini zinapanda. Akizungumza na uongozi na wafanyakazi wa tume hiyo alipozuru ofisi zake, Dk Kijaji alisema katika kipindi cha hivi karibuni bei ya bidhaa sokoni imekuwa haitabiriki ikipanda mara kwa mara huku kukiwa hakuna dalili za kushuka kwake na hivyo kuleta sintofahamu kwa wananchi.

“Inashangaza kuona bei leo ipo hapa kesho ipo hapa, na ikishapanda haijawahi kushuka, tume ya ushindani mnatuambia kipi kilichosababisha bei ya vifaa vya ujenzi ikapanda, Watanzania tunatamani kusikia, wenye serikali yao waliotukabidhi ilani wanatusubiri”-amesema Waziri Kijaji na kuongeza 

“Je, bei tunayolipa ya saruji ndiyo tunayotakiwa kulipa Watanzania? Hili ni jukumu lako Kamishna,” alisema Dk Kijaji. Aidha, alisema anashangaa kuona vinywaji baridi vimepungua sokoni kwa zaidi ya mwezi sasa huku baadhi ya maeneo bei ya vinywaji hivyo ikipanda na tume imekaa kimya”

Waziri Kijaji amesema  hataki kuamini kama kweli kupanda kwa bei ya vinywaji hivyo kumesababishwa na mahitaji yake katika soko. Alisema katika wakati huu ambao uchumi unaendeshwa na soko huria, FCC imekuwa ni kiungo muhimu kati ya mlaji na wafanyabiashara, kwa kuhakikisha kunakuwa na ushindani katika kufanya biashara huku ikimlinda mlaji kwa kuhakikisha anapata bidhaa bora.

Alihoji sheria ya tume hiyo ya Mwaka 2003 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2020 na 2021 kama ipo sawa sawa na kama ipo sawa kwanini hayo yote yametokea na kusisitiza kuwa kama ina mapungufu katika baadhi ya maeneo wampelekee ili aweze kuipeleka bungeni kwa ajili ya kuifanyia marekebisho.

Aidha amewataka  kuhakikisha wanafanya tafiti za mara kwa mara katika maeneo mengi ili kubaini changamoto zilizopo badala ya kukaa hadi kusubiri tatizo litokee ndipo wafanye tafiti. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tume ya Ushindani (FCC), William Erio amesema tume hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake mbalimbali kwa kasi ili kumlinda mlaji na katika kipindi hicho pia wameendelea kupambana na bidhaa bandia ambapo katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2021, walifanya ukaguzi katika maeneo ya bandari kuu na bandari kavu na kukagua jumla ya makontena 2,831 ambapo kati yake makontena 58 waligundua yamekiuka taratibu kwa kuwa na bidhaa zisizofaa.

Tume ya Ushindani (FCC) ni chombo cha serikali cha kusimamia uchumi wa soko, ambapo usimamizi huo unazingatia misingi ya ushindani, kumlinda mlaji na udhibiti wa bidhaa bandia. 

Tume hii imeanzishwa chini ya kifungu namba 62 cha sheria ya ushindani namba nane ya mwaka 2003.