Search
Close this search box.
Africa

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepokea mapendekezo kutoka kwa wananchi wa tarafa za Loliondo, Ngorongoro na Sale kuhusu namna bora ya kulinda uhifadhi wa maeneo hayo nchini humo.

Wawakilishi wa wakazi wa wilaya hiyo wakiwemo Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai, malaigwanani, madiwani, wenyeviti wa vijiji, wawakilishi wa wanawake na vijana waliwasilisha maoni hayo ofisini kwa Waziri Mkuu, Mlimwa, Dodoma.

Baada ya kupokea mapendekezo hayo, Majaliwa aliwasisitiza wananchi hao waendelee kuiamini serikali kwa kuwa haiwezi kuwa na mipango mibovu kwa wananchi wake.

“Msisikilize maneno maneno ya watu wa pembeni,” alisema Waziri Majaliwa.

Akizungumzia kuhusu eneo la Msomera lililoko wilayani Handeni, Tanga yanapoandaliwa makazi kwa ajili ya kuwahamishia wakazi wa Ngorongoro waliokubali kuhama kwa hiari, Majaliwa alisema ujenzi wa nyumba za makazi 103 upo mbioni kukamilika na pia Serikali imepanga kuongeza nyumba nyingine, lengo likiwa ni kufikia nyumba 500 kwa ajili ya wakazi hao. 

Kadhalika alisema serikali inaendelea kuimarisha sekta ya mifugo ili kuhakikisha wafugaji wote nchini wanapata tija kupitia shughuli hiyo.

Hivi karibuni mamlaka za juu nchini Tanzania, zilitangaza hatua kadhaa ikiwemo kuwaondoa watu wa jamii ya wamasai wanaoishi eneo hilo kwa hiari na kuhamia maeneo jirani ambayo yametengwa maalum kwa ajili yao.

Mgogoro mkubwa kuhusu eneo hili ni kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na athari zake kimazingira na wanyamapori.

Jamii ya Wamasai wamegawanyika katika makundi mawili, wapo ambao wamekubali kuwa idadi yao ina athari kwa uhifadhi katika eneo hilo. Lakini baadhi yao hawakubali wala hawaoni tatizo la wao kuishi na kuongezeka katika eneo hilo.

Serikali ya Tanzania tayari imeanza zoezi la kuwaondoa kwa hiari wale wote watakaomua kujiandika na kuondoka eneo la hifadhi na hadi sasa zaidi ya watu 400 wamejiandikisha na wengine tayari wameshakwenda eneo lililopangwa na serikali kama makazi mapya.

Comments are closed