Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iandae semina kwa wabunge wote ili kuwajengea uewelewa wa pamoja juu ya yanayoendelea katika hifadhi ya Ngorongoro kwani wapo wabunge wanaoelewa kuhusu mgogoro huo na wapo ambapo hawajui kinachendelea
Majaliwa ametoa maagizo hayo bungeni jijini Dodoma, wakati alipochangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2021, inayoonesha kuwa idadi ya watu na mifugo imeelendelea kuongezeka kwenye eneo hilo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
“Huku tukiwa tunazungumza na wananchi kule, naiagiza Wizara ya Maliasili kufanya semina siku moja kwa wabunge wote, ili wizara iwaambie kuna nini kule Ngorongoro nini kilikuwepo awali na ni hali gani ambayo iko sasa, ili tuwe na uelewa wa pamoja hata hayo mapendekezo ya Mh. Waziri ya kutaka kuja kubadilisha mnaweza kuunga mkono au kutokuunga mkono baada ya kujua nini kinaendelea kule Ngorongoro”
Waziri Majaliwa amesema mgongano mkubwa uliopo katika hifadhi hiyo ya Ngorongoro na Loliondo unatokana na sheria zilizopo lakini pia yapo masilahi binafsi ya mtu mmoja mmoja
“Nimesikiliza mjadala unaogusa maeneo ya Ngorongoro na Loliondo juu ya mahitaji makubwa ya uhifadhi wa maeneo hayo kwa maslahi ya taifa , ni kweli upo mgongano mkubwa unaotokana na sheria tulizonazo, lakini pia matakwa binafsi ya mtu mmoja mmoja” amesema Waziri Majaliwa.
Hata hivyo amesema atafanya mkutano na wananchi wa Ngorongoro na wananchi wa Loliondo licha ya kuwa mikutano hiyo ilishafanywa mara kadhaa katika kipindi cha mwaka 2017/18.
“Nitafanya mikutano na wananchi wa eneo la Ngorongoro, nitafanya mikutano na wananchi wa eneo la Loliondo ambako pia mwaka 2017/18 tumefanya mikutanao mingi sana kueleweshana juu ya jambo hili. Lakini haya yote haya na mjadala unaoendelea hapa Bungeni, wako ambao wanaelewa mazingira yaliyoko kule lakini wako wabunge ambao hawajui mazingira yaliyoko pale.”amesema Waziri Majaliwa.
Aidha Majaliwa amesema kutokana na kinachoendelea huko Ngorongoro na Loliondo, kwa hatua hizo za kuzungumza nao na kufanya mabadiliko ya sheria kutasaidi kuumaliza kwa amani mgogoro kadri itakavyoamuliwa.
Hivi karibuni kuliibuka tena mjadala juu ya wananchi wanaokaa karibu na hifadhi hizo kwamba wanatakiwa kuondolewa kutokana na wingi wao ili kulinda mazingira na wanyama wa eneo hilo, jambo ambalo linapingwa na wakazi wa huko kwa kile walichodai kuwa kwanini wamesubiri hadi wamewekeza katika maeno hayo na ndipo sasa wawaondoe.