Wakili wa kujitegemea Dikson Matata amesema wameweka nia ya kumfungilia kesi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa kwa kuvunja nyumba ya mteja wake kinyume na sheria.
Matata anamuwakilisha ndugu Johnsen Leornard Mahururu ambaye hivi karibuni amebomolewa nyumba yake ya ghorofa moja lililopo kwenye eneo la kiwanja no. 484 Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Wakili Matata amesema kitendo kilichofanywa na Waziri Silaa kutoa agizo na kusimamia zoezi la ubomoaji wa nyumba hiyo ni kinyume na sheria kwani wakati zoezi hilo linafanyika mteja wake(Leornard Mahururu), hakuwahi kupewa notice ya kubomoa kama sheria ya ardhi inavyotaka.
“Siku hiyo majira ya mchana Waziri wa Ardhi akiwa ameambatana na mkuu wa wilaya pamoja na wafanyakazi wa idara ya ardhi kutoka manispaa ya kinondoni, akiwa pia na polisi wenye mitutu na gleda, walivamia eneo la mteja wangu alimaarufu kama ghorofa la kifahari na kulibomoa” amesema Wakili Dikson Matata
Matata anasema kwa sasa wnafungua kesi dhidi ya Jerry Silaa ya kumtaka kulipa zaidi bilioni 20 kama fidia ya mali za Mahururu na kitendo cha kumzalilisha mteja wake kwa kuitwa tapeli
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi ni kwamba Mahururu hakuwa na nyaraka za umiliki wa eneo hilo na pia hakua na kibali cha kujenga hapo na kwamba Mahururu alivamia eneo hilo ambalo linamilikiwa na bi Naomi Raymond ambaye anadaiwa kulipigania eneo hilo kwa takribani miaka 20 sasa.
Kwa sasa Mahururu anashikiliwa na Jeshi la Polisi kituo cha Oysterbay ambapo alikamatwa jijini Dodoma Machi 16,2024 akiwa katika shughuliu zake na kisha kusafirishwa hadi Dar es salaam kituo cha Oysterbay.
Hata hivyo kwa mujibu wa Wakili Matata tangu siku hiyo si wanasheria wa mtuhumiwa wala ndugu walioruhusiwa kumuona bwana Maruru jambo linalowapa shaka kutokana na mwenendo wa jambo hilo linavyokwenda.
Sheria inataka mtuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24 tangu muda aliokamatwa lakini hilo ni tofauti ambapo ni zaidi ya siku tano tangu Johnsen Maruru akamatwe.
Matata anasema wana fununu kwamba huenda mteja wao akapewa kesi ya uhujumu uchumi na jitihada ya Waziri Silaa kumnyamazisha mteja wao asiendelee kudai haki yake.
Kutokana na hilo Matata amesema tayari wameandika maombi kwenda Mahakamani kuitaka itoe amri kwa Polisi na yeyote anayemshikilia Mahururu kumleta Mahakamani ili aweze kupata dhamana maombi ambayo yapo kwa jaji Mwaigogo
Maruru anawakilishwa na mawakili watatu wakiongozwa na Wakili Dickson Matata.
Sakata la mgogoro hilo limedumu kwa takribani miaka 20, ambapo limepita katika ngazi mbalimbali za Serikali na Mahakama na hatimae kutolewa uamuzi wa kumilikishwa kwa eneo hilo kwa bwana Johnsen Mahururu