Waziri Ummy azitaka hospitali za Rufaa kuboresha huduma za afya

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amezitaka hospitali za rufaa za mikoa kuboresha huduma za afya na miundombinu ya hospitali hizo ili kuipunguzia majukumu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika utoaji wa huduma.

Ummy amesema hospitali hizo zinapaswa kuboreshwa huduma ili zilingane na mahitaji ya wananchi kwani hospitali hizo zinaaminiwa.

“Tunatakiwa kuhakikisha utoaji wa huduma za afya ni mzuri, hivyo ni wakati wa kuangalia changamoto na kuziboresha ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wanafika kwenye vituo vyetu kupata huduma,” amesema Ummy.

Aidha, Waziri huyo ameitaka idara hiyo kufanya upya mapitio ya miongozo ya utoaji huduma ili kufanya huduma zinazotolewa kuanzia ngazi ya zahanati hadi Taifa zinakuwa bora na zenye manufaa kwa wananchi, vilevile miongozo hiyo iweze kuunganisha  vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Waziri Ummy amewataka watumishi wa idara hiyo kufanya kazi kama timu na endapo kuna changamoto ni vyema zikajadiliwa kwa pamoja ili kwenda kwa pamoja katika kuboresha huduma za afya nchini.