Uchumi wa Tanzania umetajwa kuongezeka kwa asilimia 0.1 baada ya kukua kwa asilimia 4.9 katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2021, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.
Waziri wa Fedha na Mipango nchini Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, ameyasema hayo wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/23 na mfumo na ukomo wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/23.
“Uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2021 ukuaji wa uchumi wa Taifa ulikuwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020,” Dk.Mwigulu
Aidha Dk Mwigulu amesema ujazi wa fedha ulikua kwa wastani wa asilimia 10.2 mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 8.8 mwaka 2020 huku riba ya mikopo ikipungua na kufikia wastani wa asilimia 16.59 mwaka 2021 ikilinganishwa na asilimia 16.66 mwaka 2020.
Amesema mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 10 Desemba 2021 ikilinganishwa na asilimia 3.1 Desemba 2020.
Kwa mujibu wa Waziri huyo akiba ya fedha za kigeni ilikuwa dola za Marekani bilioni 6.4 Desemba 2021, kiasi kinachotosheleza kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6.6, ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 6.0, zilizotosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 5.6 Desemba 2020.