Waziri wa mambo ya ndani Tanzania ashangazwa na watu kuhusisha siasa na utekaji unaoendelea nchini humo.

 

Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni amesema katika kipindi cha mwaka huu kuanzia Januari hadi kumetokea matukio nane ya utekaji na asilimia kubwa ya watuhumiwa wa utekeji huo wamekamatwa na kufikishwa mahakamani.

 

Waziri Masauni ametoa kauli hiyo leo katika uzinduzi wa kitabu cha Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar Zuberi huku akishangazwa na namna ambavyo siasa imekuwa ikitumika katika matukio hayo kwa kuyahusisha na vyombo vya dola ambavyo jukumu lake ni kulinda Raia na mali zao.

 

Amesisitiza kwamba vyombo vya dola vinauwezo wa kutosha kuwakamata watuhumiwa wote wa utekaji na kudhibiti matukio hayo.

 

“Matukio ya watu kutekwa nchini Tanzania tangu Januari 2024 hadi leo hayazidi manane tu,”amesema Waziri Masauni

 

Kauli ya Masauni imekuja wakati ambapo kumetokea tukio la hivi karibuni la kijana maarufu Sativa, ambaye anadaiwa kutekwa na wasiojulikana na kisha kutupwa katika msitu wa Hifadhi ya Katavi.

 

Sativa ambaye anaendelea na matibabu katika hospitali ya Agha Khan anadaiwa kupotea tangu Juni 23 na kupatikana Juni 27, katika msitu huo akiwa katika hali mbaya.

 

Katika maelezo yake Sativa anadai alitekwa na wasiojulikana na kisha wakampeleka katika karakana ya kituo cha Polisi Oysterbay Dar es salaam kabla ya kupelekwa mkoani Katavi.

 

Baada ya kupatikana katika hali hiyo ikapitishwa harambee kwa ajili ya matibabu yake kutoka kwa wafuasi wa mtandao wa twitter na wadau wengine wa haki nchini Tanzania.

 

Hata hivyo taarifa zinaeleza kwamba Rais Samia atagharamia matibabu yote ya Sativa pamoja na uchunguzi wa tukio hilo.

 

Mbali na tukio hilo la Edgar Mwakabela(Sativa), lililotokea Juni 23,2024, tukio lingine kama hilo ni la mtoto Asimwe Novart mwenye ualbino aliyechukuliwa mikononi mwa mama yake na wasiojulikana kabla ya kupatikana kwa mwili wake ukiwa umekatwa viungo Juni mwaka huu.

 

Katika tukio la kutekwa na kuuawa kwa mtoto Asimwe watu tisa akiwemo baba mzazi wa mtoto huyo wanashikiliwa.

 

Visa vya utekaji vimekuwa vikitisa vichwa vya habari nchini Tanzania huku bado kukiwa na sintofahamu ya anaehusika na matukio hayo.

 

Hadi sasa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kuhusu watekaji na mamlaka nazo bado hazitoa taarifa kamili juu ya ukomeshwaji wa matukio hayo

 

Kuna visa vingi ambavyo vimewahi kutokea hasa katika Serikali ya awamu ya tano ndio vilionekana kutikisa zaidi.

Baadhi ya waliotekwa na kutekwa na kuteswa bado wana hadhithi za kusimulia lakini kinachowaumiza hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyeshikiliwa na polisi hali inayowafanya kuogopa maisha yao.

Mwanaharakati maarufu nchini, Mdude Nyagali, ni miongoni mwao, wengine ni msanii maarufu Roma Mkatoliki ambaye hivi sasa anaishi ughaibuni lakini pia bilionea  Mohammed Dewji na wengine.

Baadhi walifanikiwa kurudi wengine mpaka sasa ni story tu imebaki mfano hadi sasa haijulikani alipo mwanahabari Azory Gwanda, Ben Saanane na wengine.

Pia taarifa zilizoleta maswali mengi ambayo hadi sasa hayana majibu ni kupotea kwa vijana watano waliopotea kwa mazingira ya kutatanisha licha ya ndugu kutoa taarifa polisi lakini hadi sasa hawajafanikiwa kuwapata ndugu zao.

Matukio ya mauaji, utekaji na utesaji yamekuwa yakihusishwa moja kwa moja na siasa nchini Tanzania na mara kadhaa yameonekana kushamir kila baada ya uchaguzi mmoja kwenda uchaguzi mwingine mwengine.