Waziri wa zamani nchini Tanzania Geofrey Mwambe ashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za jinai

Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limekiri kumshikilia waziri wa zamani, Geofrey Mwambe, tangu usiku wa tarehe 7 Desemba 2025, baada ya kukamatwa katika eneo la Tegeta, wilayani Kinondoni, kutokana na tuhuma zinazohusiana na makosa ya jinai ambayo bado hayajafafanuliwa na yanaendelea kuchunguzwa.

Taarifa ya polisi iliyotolewa leo, tarehe 12 Desemba 2025, imeeleza kuwa Mwambe ambaye aliwahi kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na baadaye Wizara ya Viwanda na Biashara alikamatwa wakati wa operesheni ya kawaida ya kufuatilia masuala ya usalama jijini Dar es Salaam. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua za awali za kisheria kuhusu tuhuma zinazomkabili zinaendelea kukamilishwa.

Mwambe, aliyewahi pia kuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) na Mbunge wa Masasi mkoani Mtwara (CCM), amekuwa akiendelea kushikiliwa tangu Desemba 7. Baada ya ukimya kuibuka kuhusu kuzuiliwa kwake, jana tarehe 11 Desemba 2025, IGP, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) pamoja na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO) walifunguliwa shauri mahakamani wakituhumiwa kumshikilia kinyume cha sheria.

Shauri hilo, lenye namba 289778/2025, limewasilishwa na Mwambe kupitia wakili wake, Hekima Mwasipu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya hati ya dharura, na limepangwa kusikilizwa tarehe 15 Desemba 2025.

Katika taarifa hiyo, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu huku likikamilisha taratibu za uchunguzi na mchakato wa kisheria.

Hatua hii inakuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, kulitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha taratibu za ukamataji zinazingatia sheria na kufanyika kwa staha.