Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amekerwa na wezi wa miundombinu ya barabara katika miradi inayoendelea na kulaani vikali vitendo hivyo.
Akizungumza leo Mei 18, 2022 katika ufunguzi wa barabara ya Tabora, Koga – Mpanda KM 342.9, Rais Samia amesema miundombinu hiyo inatengenezwa kwa fedha nyingi za mikopo.
Amesema barabara ya Tabora, Koga Mpanda imejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa gharama ya Sh bilioni 473.879 .
“Viongozi na wananchi jana nilisisitiza kuhusu kulinda miundombinu, lakini nimesikitishwa katika mradi unaondelea kuna watu wameng’oa nguzo za taa za barabarani na kuiba panel tisa za sola katika kijiji cha Kasandalala, Tumbili Usenga na Sikonge Mjini.
“Huu ni uhujumu uchumi, nimetaja mabilioni tunayokopeshwa, ili tufanye miradi hii, mtu kwa utashi wake anakwenda kung’oa nguzo, ili apate panel ya sola, inampeleka wapi? Itamfaa nini? Hata ukiitumia nyumbani kwako hutoitumia muda mrefu,” amesema.
“Watu wanaofanya uhalifu huu mnakaa nao majumbani, naomba sana toeni taarifa polisi za wahalifu hawa,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Rais Samia Sameiagiza Wizara ya Ardhi itumie vyema ardhi kwa kupanga matumizi bora itumike kama ilivyokusudiwa.
Aamewataka wafugaji kubadilika na kuwa na mifugo yenye tija, badala ya kuona fahari kuwa na mifugo mingi isiyowaletea tija wala maendeleo.
“Si wakati wa kuona fahari, niwaombe Wanyemwezi na Wasukuma wenzangu huu si wakati wa kukaa na ng’ombe wengi ambao hawakuletei faida, kukaa na ng’ombe wengi wasio na faida si zama hizi, kwani wanasababisha kuhitaji ardhi kubwa na kuharibu vyanzo vya maji na kuharibu mazingira pamoja na kukosekana mvua kutokana na ukataji miti.Tubadilike,” amesema.
Amewataka Wizara ya Ardhi na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Taasisi ya Misitu (TFS) kukaa na kupanga matumizi mazuri ya ardhi, ili kilimo kiwepo, uvuvi uwepo na ufugaji uwepo mvua ipatikane na maendeleo yapatikane bila kuharibu mazingira.
“Nina taarifa za wavuvi kwenye mto Ugala kuwa maofisa wanatengeneza mazingira ya rushwa kwa kuwazuia watu kuvua ili wale wanaotoa fedha ndio wanaruhusiwa kuvua, naomba wizara husika iliangalie suala hilo ipasavyo,” amesema.