Shirika la afya duniani WHO limetahadharisha kuwa hatua za haraka zinahitajika ili kukabiliana na ongezeko la ugonjwa wa kipindupindu.
Tahadhari hiyo imetolewa katika wakati ambapo dunia inakabiliwa na uhaba wa chanjo dhidi ya ugonjwa huo wa kuharisha.
Shirika la kimataifa la kuratibu usambazaji wa chanjo ICG, limesema mamilioni ya watu wanakabiliwa na hatari ya kupata kipindupindu kwa sababu kampuni pekee inayozalisha chanjo dhidi ya ugonjwa huo, EuBiologics ya Korea Kusini, imelemewa na mahitaji.
Kupitia taarifa, shirika hilo limeeleza kuwepo kwa ongezeko la wagonjwa wa kipindupindu duniani kote.
ICG imeongeza kuwa, uzalishaji wa chanjo duniani mwaka huu utakuwa kati ya dozi milioni 17 na milioni 50 japo idadi hiyo huenda ikawa ndogo ukilinganisha na mahitaji ya wagonjwa.