Shirika la Afya duniani, WHO, limeripoti uwezekano wa kuweko kwa mlipuko wa homa ya Marburg wilayani Biharamulo na Muleba, mkoani Kagera nchini Tanzania baada ya watu 9 kuugua wakiwa na dalili zinazofanana na za ugonjwa huo ambapo kati yao 8 wamefariki dunia.
Kupitia ukurasa wake WHO imesema hadi tarehe 10 mwezi huu kulikuwa na wagonjwa 6 lakini idadi iliongezeka na kufikia 9 tarehe 11 mwezi huu na wagonjwa walikuwa na dalili kama vile maumivu ya kichwa, homa, maumivu ya mgongo, kuhara, kutapika damu, uchovu wa mwili na mwishoni kabisa ni kutoka damu kwenye matundu yote ya mwili.
Homa ya Marburg huambukizwa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu mwingine kupitia majimaji au damu ya mtu aliye na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jumatatu tarehe 13, Januari, WHO iliarifu nchi wanachama kuhusu uwezekano wa mlipuko huo wa homa ya Marburg katika wilaya za Biharamulo na Muleba mkoani Kagera.
Tayari sampuli kutoka kwa wagonjwa wawili zimekusanywa na kufanyiwa uchunguzi kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Umma nchini Tanzania na majibu yanasubiriwa ili kuthibitisha iwapo ni homa ya Marburg au la.
Waambata wa wagonjwa hao pamoja na wahudumu wa afya katika wilaya hizo mbili ambao waliwahudumia wameshabainishwa na wanafuatiliwa.
Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera kwa mara ya kwanza ilikumbwa na mlipuko wa homa ya Marburg mwezi Machi mwaka 2023, ambapo mazingira na wanyama wanaosababisha maambukizi kama vile popo bado wako eneo hilo.
Mlipuko huo wa 2023 uliokumba wagonjwa 9 na sita kati yao kufariki dunia, ulidumu kwa miezi miwili.
Hatua za afya ya umma
Tayari timu ya kitaifa ya kuchukua hatua imepelekwa kusaidia uchunguzi na hatua dhidi ya mlipuko huo unaoshukiwa; halikadhalika juhudi za usimamizi na ufuatiliaji zimeimarishwa sambamba na kufuatilia waambata.
Kliniki tembezi imeanzishwa mkoani Kagera pamoja na vituo vya matibabu.
Tathmini ya WHO kuhusu hatari ya sasa
Katika kiwango cha kitaifa, WHO inasema hatari ya ugonjwa huo kutokana na vigezo kadhaa kwa kuzingatia kati ya washukiwa 9, tayari 8 wamefariki dunia wakiwemo wahudumu wa afya na chanzo hakijajulikana.
Vile vile ripoti ya washukiwa wa ugonjwa wa Marburg kuweko katika wilaya mbili tofauti, kunadokeza kusambaa kwa virusi hivyo kwenye maeneo tofauti kijiografia.
Kikanda pia kuna hatari kubwa ya kusambaa kutokana na mkoa wa Kagera kuwa eneo la mpito na harakati za mipakani katika nchi za Rwanda, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Baadhi ya wagonjwa washukiwa walioripotiwa wanaishi kwenye wilaya zilikoko mpakani na hivyo hatari ya kusambaa nchi jirani.
Kimataifa hatari ni ndogo na hakuna pendekezo la vizuizi
Hatari ya kusambaa kimataifa, kwa mujibu wa WHO, bado ni ndogo kwani hakuna uthibitisho. Hata hivyo ufuatiliaji wa karibu unatakiwa mipakani.
Ni kwa mantiki hiyo WHO inasema kwa kuzingatia tathmini ya sasa hakuna tahadhari yoyote ya kuzuia usafiri kwenda Tanzania au biashara na taifa hilo.