WHO:Watu milioni 8 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na tumbaku

Ikiwa leo ni siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani shirika la Umoja wa Mataifa  la afya duniani WHO, limezitaka nchi kuacha kutoa ruzuku kwa kilimo cha tumbaku na badala yake kuunga mkono na kusaidia kilimo cha mazao endelevu yatakayoweza kulisha mamilioni ya watu wenye uhitaji wa chakula.

Kupitia ujumbe wake wa siku hii mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema “Tumbaku inawajibika kwa vifo milioni 8 kila mwaka  lakini bado serikali duniani kote zitatumia mamilioni ya dola kuunga mkono mashamba ya tumbaku. Watu duniani kote wanakabiliwa na njaa wakati ekari milioni 300 za dunia yetu zinatumika kulima tumbaku.”

Akaenda mbali zaidi na kusistiza kwamba “Ni wakati wa kubadili mwelekeo wa juhudi zetu na kujikita na kilimo ambacho kinastawisha siha yetu na mazingira yetu.”

Hivi sasa kwa mujibu wa WHO zaidi ya watu milioni 300 duniani kote wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na uhakika wa chakula wakati ambapo zaidi ya ekari milioni 300 katika nchi zaidi ya 120 duniani zinatumika kulima tumbaku hata kwenye nchi ambazo watu wana njaa kali.

Dkt. Tedros amesema WHO inafanyakazi kwa karibu na mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa likiwemo la chakula na kilimo FAO na la mpango wa chakula duniani WFP kuwasaidia wakulima kuhamia kwenye kilimo mbadala wa tumbaku kwani “kwa kuchagua kulima chakula badala ya tumbaku tutatoa kipaumbele kwa afya, kulinda mfumo wa maisha na kuimarisha uhakika wa chakula kwa wote.”

Lengo la maadhimisho ya mwaka huu ni kuujulisha umma hatari za matumizi ya tumbaku, mwenendo wa biashara wa makampuni ya tumbaku, nini kinachofanywa na WHO kupambana na janga la tumbaku na nini watu duniani kote wanaweza kufanya ili kudai haki yao ya afya,  maisha yenye afya na kuvilinda vizazi vijavyo.

Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani huadhimishwa kila mwaka Mei 31 na mwaka huu imebeba maudhui “Lima chakula sio tumbaku.”