Search
Close this search box.
Africa

Yaliyojiri kesi ya Freeman Mbowe

13

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA


Kesi ya Freeman Mbowe hivi sasa inaendelea kusikilizwa katika Mahakama Kuu Division ya Makosa ya Rushwa na
Uhujumu Uchumi jijini Dar es salaam.

Kesi hiyo yenye mvuto mkubwa tangu kuanza kusikilizwa kwake, imebeba hisia za waliowengi hasa wanasiasa wa
vyama vya upinzani kutoka ndani na nje ya Tanzania, Wanaharakati lakini kubwa zaidi ni kesi inayofatiliwa
kimataifa.

Mbowe anashtakiwa kwa makosa ya Ugaidi na Uhujumu Uchumi, kesi ambayo kwa mujibu wa sheria za Tanzania
kesi hiyo haina dhamana. Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo kupitia chama cha CHADEMA, hivi sasa jina lake limezidi kuwa maarufu katika uga wa siasa kutokana na misimamo yake mikali anayoiyamini katika kupigania haki za wananchi.

Amekuwa mwiba wa serikali iliyopo mamlakani na amekuwa kivutio kikubwa cha wanachama wake wa
CHADEMA ambao hivi sasa kutwa kucha maskani yao makubwa ni katika viunga vya mahakama yoyote
ambayo Mbowe anapelekwa.

LAKINI KWANINI FREEMAN MBOWE HIVI SASA ANAKABILIWA NA KESI YA UGAIDI?


Mnamo Julai 21, 2021 Mbowe na wenzake 10 walikamatwa na Polisi jijini Mwanza akiwa katika
maandalizi ya kuhudhuria mkutano wa Kongamano la Katiba na kisha kupelekwa kusikojulikana hali iloiyozua
sintofahamu.

Kufuatia sintofahamu hiyo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kikalitaka jeshi la polisi kutoa
taarifa za wapi kiongozi wao alipo lakini baada ya takribani siku mbili mbele Kamanda wa Polisi mkoani
Mwanza Ramadhan Ng’anzi alisema walikuwa wakimzuilia Mbowe kwa mahojiano zaidi hata hivyo wakapata taarifa
kutoka Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam kuwa Mbowe anatakiwa kufikishwa jijini Dar es salaam kwa ajili ya mahojiano mengine kutokana na tuhuma anazokabiliwa nazo.

Mara baada ya taarifa hiyo Mbowe alifikishwa jijini Dar es salaama, na ilipofika Julai 26, 2021 alipandishwa
kizimbani kwa mara kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam kwa tuhuma za vitendo
vya  ugaidi.

Freeman Mbowe akiwasili katika Mahakama Kuu Division ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es salaam.


Katika kesi hiyo Mbowe alikuja kuunganishwa na wenzake wengine watatu wanaodaiwa kushirikiana nae ambapo
Agosti 23, 2021 walisomewa mashtaka sita likiwemo la kutaka kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai
wakati huo, Lengai Ole Sabaya.

Washtakiwa hao aliounganishwa nao katika kesi hiyo walikuwa ni walinzi watarajiwa wa Mbowe aliopanga
kuwaajiri ambao Halfan Bwire Hassan, Adam Hassan Kasekwa na Mohamed Abdallah Ling’wenya.

Hata hivyo kesi hiyo ikaamishiwa katika Mahakama Kuu Division ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,
kutokana na Mahakama ya Kisutu kutokuwa na sifa ya kusikiliza shauri hilo.Septemba 3, 2021 kesi hiyo ikaanza kusikilizwa rasmi katika  Mahakama hiyo mbele ya Jaji Elinaza Luvanda, ambaye baadae alijiondoa kwenye kesi hiyo baada ya washtakiwa kukosa imani nae.


Baada ya kujiondoa jaji Luvanda kesi hiyo ikapangiwa jaji mwingine ambaye hadi sasa ndiye anayeendelea
kusikiliza shauri hilo Jaji Muspha Siyani. Kwa sasa hatua iliyofikia kwenye kesi hiyo ilikuwa
inasikilizwa kesi ndogo ndni ya kesi kubwa ya Msingi Na 16/2020.ambayo Jopo la mawakili wa utetezi likiongozwa
na wakili Peter Kibala walipinga maelezo ya onyo yaliyotolewa na mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa.


MASHAHIDI WALIVYOTOA USHAHIDI


Kesi hiyo ndogo imesikilizwa kwa kutolewa ushahidi wa mashahidi sita kutoka upande wa serikali na utetezi ambapo ushahidi huo ulimazika septemba 29.

Katika mashahidi hao sita, watatu ni mshahidi wa upande wa utetezi na wengine watatu ni wa upande wa serikali.
Septemba 15, 2021 Mahakama ilianza kusikiliza ushahidi kutoka kwa mashahidi wa upande wa serikali ambapo
mashahidi hao walikuwa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhani Kingai na Inspekta wa
Polisi Mahita Omari Mahita.

Katika ushahidi wa mashahidi wa upande wa serikali miongoni mwa yaliyosemwa na mashahidi hao waliiambia
mahakama kwamba waliwakamata washtakiwa wakiwa na silaha aina ya bastola na  kete 25 za dawa za kulevya.
Mashahidi hao pia wameileza Mahakama kuwa walipata taarifa za uhalifu kwamba kuna kuna watu wamepanga
kufanya vitendo vya kigaidi kwa kulipua vituo vya mafuta katika maeneo mbalilmbali ya nchi ikiwemo Arusha,
Morogoro na Dar es salaam.


Pamoja na mambo mengine mashahidi hao wameelezea namna ambavyo walivyowakamata watuhumiwa ambao
ni Adam Kasewkwa na Mohamed Lingwenya, wakiwa Moshi eneo la Rau Madukani mkoania Kilimanjaro na
kisha kuwapeleka kituo cha polisi Moshi na baada ya hapo kuwasafirisha hadi jijini Dar es salaam.
Mashahidi kwa ujumla walipoulizwa na mawakili wa pande zote mbili kuhusu kuwatesa watuhumiwa wakiwa
chini yao, walikana na kusema hawakuwatesa isipokuwa walihudumiwa vizuri kama ambavyo mtuhumiwa anapaswa kuhudumiwa.


Baada ya kusikiliza hayo yote ushahidi wa upande wa serikali ukafungwa na kurusu mashahidi wa upande wa utetezi kutoa ushahidi wao, ambapo mashahidi wa upande huu walikuwa ni mshtakiwa wa pili  Adam
Kasekwa, mshtakiwa wa tatu Mohamed Ling’wenya na mke wa mshtakiwa wa pili aliyejitambulisha kwa majina
ya Liliani Furaha Kibona.

Ushahidi uliotolewa na mashahidi hawa wa utetezi hususani shahidi wa kwanza na wa pili, ulielezea mateso
waliyoyapata watuhimiwa wakiwa mikononi mwa jeshi la polisi, ikiwemo kupigwa hadi kwasababishia maumivu
kwenye miguu.

Wa kwanza kulia ni Freeman Mbowe wa pili ni Halfan Bwire wa tatu ni Mohamed Ling’wenya na wan ne ni Adama kasekwa. Pia ushahidi huo ulieleza kwamba shahidi wa pili ambaye ni mshtakiwa wa tatu Mohamed Lingwe’nya alidai
kwamba hakupata chakula cha mahabusu kama iinavyotakiwa kwa takribani siku 10 akiwa mahabusu ya
kituo cha Mbweni jijini Dar es salaam, na badala yake alikuwa akipewa biskuti, maji, na hata juice na askari
mmoja ambaye jina hakumtaja ambapo amesema huyo askari alikuwa amezoeana nae tangu alipofikishwa katika
kituo hicho.

Kwa upande wa shahidi wa tatu ambaye ni mke wa Kasekwa, Liliani Furaha Kabona amedai kwamba
walifunga ndoa na mume wake kwa taratibu za kiserikali mwaka 2016, wakati huo mume wake akiwa ni mtumishi
wa Jeshi la Wananchi Tanzania, kikosi cha makomandoo 92KJ, kilichopo Ngerengere mkoni Morogoro, lakini kwa
sasa ameachishwa kazi hiyo.


Shahidi huyo alidai kwamba baada mume wake kuachishwa kazi, aliamua kufanya biashara zake
ndogondogo, lakini siku moja alipigiwa simu na rafiki yake aitwaye Ling’wenya kuwa kuna kazi ya ulinzi kwenda
kumlinda kiongozi wa CHADEMA Freeman Mbowe hivyo walitakiwa kwenda Moshi.

Baada ya mazungumzo hayo walikubaliana siku ya kuondoka, na baada ya kufika huko mume wake alikua
anawasiliana nae kwa njia ya simu, lakini ilipofika tarehe 5 Agosti 2020, mawasiliano yalikata, na kila alipojarubu
kumpigia simu ya mume wake haikuwa inapokelewa na ilifika wakati ikawa haiti kabisa. Ndipo alipoona kuna haja
ya kumtafuta Ling’wenya ambaye walikua wote Moshi lakini na yeye hakua anapokea simu.


Alikuja kupata taarifa kwamba mume wake alikamatwa akiwa Moshi, lakini amesafirishwa jijini Dar es salaam.Taarifa hizo alizipata kwa mke wa Ling’wenya ambaye aliwasiliana nae kujua kama anataarifa zozote.

Shahidi huyo aliendelea kuiambia Mahakama kwamba yeye ni mkazi wa CHALINZE, lakini baada ya kupata
taarifa hiyo alifika Dar es salaam, na kushauriana na wenzake akiwemo mke wa Ling’wenya kwenda kumtafuta
mume wake Adam Kasekwa na mwenzake Mohamed Ling’wenya kwenye vituo vya polisi.

Alidai kuwa alizunguka vituo vya polisi vinne, ikiwemo kituo cha Central Dar es salaam, Tazara, Oysterbay na
kituo cha polisi Chang’ombe bila mafaniki.

Baada ya kuwakosa katika vituo hivyo walianza kuwatafuta katika hospitali 3, ikiwemo hospitali ya Taifa
Muhimbili, hospitali ya Mwananyama, na hospitali ya Amana nako huko hakuwapata.

Shahidi huyo aliendelea kuiambia Mahakama kwamba baada ya kuona maeneo hayo yote watu hao hawapo
aliona arudi nyumbani kwake Chalinze na kutafakari kuona atafanya nini baada ya hapo, lakini siku kadhaa
mbele alimuona mume wake na wenzake  kwenye taarifa ya habari ikieleza kwamba wanashtakiwa kwa makosa ya
ugaidi.


Shahidi akamaliza  ushahidi wake ambapo Mahakama ikaufunga ushahidi huo, na Jaji Mustapha Siyani. akaahirisha kesi hiyo hadi tarehe 19 ambapo kesi hiyo ndogo  nadni ya kesi kubwa ya msingi Na16/2020 itakapokuja kutolewa maamuzi.

Freeman Mbowe na wenzake wanatuhumiwa kwa makosa ya ugaidi, mashtaka hayo ni pamoja kula njama za
kutenda ugaidi ambapo Mbowe anatuhumiwa kufadhili vitendo hivyo vya kulipua vituo vya mafuta kwa kutoa
zaidi ya shilingi laki sita, pia Watuhumiwa wote wanatuhumiwa kushiriki vikao vya kutenda kosa la ugaidi
huku Mshtakiwa wa pili anatuhumiwa kumiliki bastola yenye risasi tatu kwa ajili ya kutenda kosa la ugaidi hna
Mshtakiwa wa kwanza akituhumiwa kumiliki nguo, begi na koti zote za Jeshi la Wananchi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

HUYU NDIYE FREEMAN MBOWE


Freeman Aikaeli Mbowe amezaliwa 14 Septemba 1961 ni mwanasiasa Mtanzania, mwanachama na mwenyekiti wa
chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, chama cha CHADEMA. Alichanguliwa tangu mwaka 2000 kuwa
mbunge wa jimbo la Hai lililopo mkoani Kilimanjaro, akarudishwa kwa miaka 2015-2020.

Alikuwa mmoja wa waasisi wa CHADEMA mwaka 1992, Mbowe anafahamika kuwa mpangaji mahiri wa mikakati,
na hivyo kumfanya kuwa mmoja wa wapanga mikakati wakuu wa CHADEMA na kiongozi wa juu kabisa. Mnamo
mwaka 2005 Mbowe aliwania uraisi wa Tanzania kupitia chama chake cha CHADEMA na kuambulia asilimia 5.88
ya kura zote.

Mnamo Julai 2021, Freeman Mbowe, alikamatwa pamoja na wanachama wengine kumi wa chama waliondoka
kwenda Mwanza (kaskazini magharibi) ambapo walikuwa wakipanga mkutano.

Comments are closed

Related Posts