Idadi ya wakimbizi wanaofungasha virago kukimbia mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine sasa imevuka watu milioni 5, kwa mujibu wa takwimu mpya zilizotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo mkubwa zaidi wa wakimbizi kushuhudiwa barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya dunia.
Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, Filippo Grandi amesema waukraine 5,034,439 wameondoka nchini mwao tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi tarehe 24 ya mwezi Februari mwaka huu.
Amesema idadi hiyo ni ongezeko la watu zaidi 53,586 ikilinganishwa na idadi iliyotolewa siku ya Jumanne.
“Watu milioni 5 sasa wameikimbia Ukraine. Wameacha nyumba na familia zao,” amesema Kamishna Mkuu Grandi katika ujumbe aliouandika jana kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Ameongeza kuwa “Watu wengi wangefanya lolote, na wengine hata wanahatarisha maisha yao ili kurudi kuwaona wapendwa wao. Lakini kila shambulio jipya linalofanyika linavunja matumaini yao. Kukomeshwa kwa vita ndio suluhu pekee inayoweza kuandaa njia bora ya kujenga upya maisha yao.”
UNHCR inasema hadi kufikia machi 30 mwaka huu watu milioni 4 walikuwa wameshakimbia Ukraine. Hata hivyo shirika hilo limeongeza kuwa kwa sasa hatua ya watu kukimbia imekuwa ya polepole katika wiki za hivi karibuni kuliko ilivyokuwa mwanzo wa vita.
Miongoni mwa wakimbizi hao milioni 5, zaidi ya wakimbizi 218,000 sio waukraine bali ni raia wa nchi nyingine, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM.