Zaidi ya watu milioni tatu ndio waliopata chanjo kamili ya UVIKO-19 Tanzania

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema hadi kufikia Machi 21, 2022 jumla ya watu milioni 3,016,551 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30,740,928 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ikiwa ni sawa na asilimia 9.81.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati akipokea msaada shehena ya chanjo ya UVIKO-19, aina SINOVAC dozi milioni moja kutoka kwa Serikali ya Uturuki

“Hadi kufikia Machi 21, 2022 jumla ya watu milioni 3,016,551 wamepata chanjo kamili kati ya watu milioni 30,740,928 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ikiwa ni sawa na asilimia 9.81”-Amesema Waziri Ummy

Hadi sasa Serikali ya Tanzania imepokea jumla ya chanjo ya UVIKO-19 dozi 10,845,774 zikijumuisha (Sinopharm, Janssen, Moderna, Pfizer na Sinovac) ambazo zinatosha kuchanja watu 6,381,327.

Waziri Ummy amesema ili kufikia kinga ya jamii ya UVIKO-19, Serikali inalenga kuchanja asilimia 70 ya Watanzania kuanzia umri wa miaka 18 hadi mwisho wa mwaka 2022, pia ametoa rai kwa wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za uhamasishaji jamii ili kuongeza kiwango cha utoaji wa chanjo.

“Nachukua fursa hii kuendelea kuwasisitiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kuendelea kutoa ushirikiano ili wananchi waendelee kuhimizwa kupata elimu ya chanjo ili wapate chanjo wajikinge na maambukizi ya UVIKO-19”. Amesema Ummy.

Pamoja na wito kutolewa kwa Watanzania kutakiwa kuchanja lakini bado kumekuwa na mdororo wa watu kujitokeza kuchanja, huku wengi wao bado wakiwa na imani kwamba chanjo hizo si salama kwao licha ya elimu kutolewa juu ya chanjo.