Mwanadiplomasia mkuu wa Urusi Sergei Lavrov amewasili Uganda katika ziara yake ya nchi za Afrika, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi alisema.
Lavrov alikaribishwa mjini Entebbe na mwenzake wa Uganda, Jeje Odongo, msemaji Maria Zakharova alisema akichapisha picha kwenye Telegram ya mawaziri hao wawili wa mambo ya nje.
Entebbe ni mji ulio karibu na mji mkuu Kampala na ndipo uwanja wa ndege wa kimataifa unapatikana.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Urusi TASS, Lavrov anatazamiwa kufanya mazungumzo siku ya Jumanne na Rais wa Uganda Yoweri Museveni.
“Rais Yoweri Museveni ambaye alizuru Urusi mara ya mwisho mwaka 2019 ametoa wito wa kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili hasa katika nyanja za ulinzi na usalama, ushirikiano wa kiuchumi na kiufundi,” serikali iliandika kwenye Twitter.
Katika kituo chake cha kwanza cha ziara mjini Cairo siku ya Jumapili, Lavrov aliwahakikishia viongozi wa Misri kwamba maagizo yao ya nafaka ya Urusi yatatimizwa.
Makubaliano hayo yanakuja baada ya makubaliano ya kihistoria kati ya Urusi na Ukraine yaliyotiwa saini siku ya Ijumaa na Umoja wa Mataifa na Uturuki yenye lengo la kuondoa mzozo wa chakula duniani uliosababishwa na kuzuiwa kwa usafirishaji wa nafaka katika Bahari ya Black Sea.
Chini ya saa 24 baadaye Moscow iligonga bandari ya Ukraine huko Odessa — mojawapo ya vituo vitatu muhimu katika usahfirishaji wa bidhaa vilivyoainishwa katika makubaliano hayo — na kuzua ghadhabu mjini Kyiv na kuzidisha hofu kwamba Kremlin haingetimiza makubaliano hayo.
Lavrov pia ametembelea Kongo-Brazzaville na baadaye anatarajiwa kwenda Ethiopia.