Mgomo wa walimu wa Zimbabwe ambao umedumaza masomo uliingia wiki ya pili siku ya Jumatatu, huku kukiwa hakuna suluhu lolote baada ya serikali kuwasimamisha kazi walimu 135,000 kwa kutoripoti kazini.
Walimu wengi hawakufika shule zilipofunguliwa kwa muhula wa kwanza wa mwaka mpya wiki jana, wakisema hawawezi kumudu tena safari hiyo.
Mwandishi wa shirika la habari la AFP ambaye alizuru shule katika mji mkuu wa Harare alikuta wanafunzi wakizunguka uwanjani au wakicheza madarasani.
Baadhi ya shule zilikuwa wazi bila walimu wala wanafunzi kuwepo.
Alhamisi iliyopita, wizara ya elimu ilisema inawasimamisha kazi walimu kwa miezi mitatu kwa kutoripoti kazini.
Vyama vya wafanyakazi vilisema baadhi ya walimu 135,000 kati ya walimu 140,000 wa shule za umma nchini Zimbabwe wamesimamishwa kazi.
âSerikali imefunga shule kwa kusimamisha zaidi ya asilimia 90 ya walimu,âTakavafira Zhou, rais wa Umoja wa Maendeleo ya Walimu wa Zimbabwe, aliiambia AFP.
Walimu nchini Zimbabwe hupata wastani wa $100 kwa mwezi.
Mgogoro wa mishahara ulianza miaka mitatu iliyopita wakati serikali ilipoacha kuwalipa wafanyakazi kwa dola za Amerika hadi dola za Zimbabwe, ambazo thamani yake imepungua kwa sababu ya mfumuko wa bei.
âMwalimu anayelipwa mshahara wa chini zaidi anapata karibu dola za Amerika 80 na tunasema tunataka kurejeshewa mshahara tuliokuwa tukipata chini ya (rais wa zamani Robert) Mugabe ambao ulikuwa dola 540,â Zhou alisema.
Alishutumu serikali kwa âkuwatendea vibayaâ walimu.
âHakuna mwalimu anayekuza pesa kwenye bustani au kupokea kama mana kutoka mbinguni,â alisema, akishutumu serikali kwa kutumia âmbinu za ujambaziâ kujaribu kuwalazimisha walimu kurejea kazini, na kuapa kwamba vyama vya wafanyakazi vitapambana na kusimamishwa kazi mahakamani.
Wakati wa utawala wa Mugabe, ambaye pia alikuwa mwalimu, Zimbabwe ilijivunia kuwa miongoni mwa nchi zenye viwango vya juu vya elimu barani Afrika.
Wanafunzi wa Zimbabwe tayari wamepoteza miezi kadhaa ya masomo kutokana na kulipuka kwa UVIKO-19.
Chama kikubwa zaidi cha upinzani cha Citizens Coalition for Change (CCC) kimelaani, madai ya kusimamishwa kazi kwa walimu… na kuendelea kupuuzwa kwa mgogoro wa malipo ya walimu na serikali.
Msemaji wa chama hicho Fadzayi Mahere alisema watoto walikuwa wahanga wa kwanza wa mzozo huo wa muda mrefu.
Aliiomba serikali kushughulikia malalamiko ya walimu ili âkuepusha kuporomoka kabisa kwa mfumo wetu wa elimu.â
âMtazamo wa serikali unaathiri pakubwa watu maskini, ambao wengi wao wana watoto wanaosoma shule za umma,â
Uchumi wa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika umekuwa ukidorora kwa zaidi ya muongo mmoja.
Migomo ya walimu, wauguzi na madaktari ni jambo la kawaida kwani wengi wanatatizika kujikimu na kudai malipo ya juu.
Rais Emmerson Mnangagwa, ambaye alichukua nafasi ya Mugabe baada ya kiongozi huyo wa muda mrefu kuondloewa katika mapinduzi, aliahidi kufufua uchumi.
Lakini wachambuzi wanasema hadi sasa ameshindwa kufanya vyema kumliko Mugabe.