Jeshi la Polisi mkoani Mtwara linamshikilia Hamis Athumani (23) mkazi wa Chigungwe wilayani Tandahimba kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi kisa kukatazwa kuomba unyumba kwa mkewe mwenye kichanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara ACP Nicodemus Katembo amesema mtuhumiwa alimuua baba yake Hamis Chipota (50) Agosti 24 mwaka huu majira ya saa 12 jioni kufuatia ugomvi wa kifamilia katika Kijiji cha Chingungwe.
“Mtuhumiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 24/08/2022 majira ya saa 12 jioni kutokana na ugomvi wa kifamilia uliozuka baada ya Mtuhumiwa kutoridhika kuelezwa na wazazi wake kuacha tabia ya kumuomba unyumba mkewe mwenye kichanga,” imeeleza taarifa ya Polisi.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo limemfikisha mahakamani Salum Bakari (59) Mkazi wa Ligula A Wilayani Mtwara kwa tuhuma za kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka 16 na kumsababishia michubuko na maumivu makali sehemu zake za siri.