TCRA yatoa sababu ya  kuitoza faini Zama Mpya Tv   

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeitoza faini ya shilingi milioni mbili chombo cha habari cha mtandaoni cha Zama Mpya kwa kosa la kuchapisha habari kuhusu tozo za serikali bila kuzingatia maadili, hivyo kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

Pia imetoa onyo na kukiweka chini ya uangalizi wa TCRA kwa miezi mitatu, ili kuboresha utendaji kazi wao.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Habi Gunze, alisema Agosti 12, mwaka huu, TCRA ilitoa leseni kwa Zama Mpya Tv na Agosti 28 mwaka huu walichapisha taarifa za uchochezi kuhusu tozo za serikali kwenye ukurasa wa twitter kinyume na kanuni ya  9 (a), 12 (a) (I) na 16 (1) aya  3 (a), (d), (g), (h) na (k)  ya kanuni za kielektroniki na Posta ya mwaka 2020.

Amesema katika utetezi wa kituo hicho,  walikiri kuchapisha habari hiyo,  huku wakieleza kuwa walitafuta na kuchapisha habari hizo kulingana na katiba na kwamba hawajui kilichochochewa na madhara yaliyopatikana.

Ameongeza kuwa TCRA ina mamlaka ya kulinda maslahi ya serikali na watumiaji wa mitandao, hivyo wana mamlaka ya kufuatilia kila taarifa inayochapishwa.

Amesema kituo hicho kimekosa umakini katika usimamizi wa maudhui, kwa sababu hawakutakiwa kuchapisha taarifa kutoka kwa mtu mmoja, bila kufuatilia na upande wa serikali.