Wakati upande wa Jamhuri leo ukiendelea kutoa ushahidi wake katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe na wenzake watatu, mvutano umeibuka katika geti la kuingia Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini Tanzania baada ya baadhi ya viongozi wa CHADEMA, waandishi wa haabri na wanachama wa chama hicho kuzuiwa kuingia ndani ya chumba cha Mahakama.
Katika mvutano huo, aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (CHADEMA) amehoji sababu za polisi kuwazuia kuingia, ili hali siku zote wamekuwa wakiingia kwa kufuata taratibu na hakuna vurugu au uvunjifu wa amani uliotokea.
Hatua hiyo imeibua mjadala mkubwa mtandano hivi sasa huku kila mmoja akitoa maoni yake kuhusu kinachoendelea mahakamani hapo.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema kinachoendelea mahakamani hapo kwenye kesi ni kama polisi wanajaribu kuzuia udhibiti wa utoaji taarifa.
“Nimetaarifiwa kwamba Polisi na/au Mahakama wanazuia watu kuingia na simu mahakamani ili kudhibiti utoaji wa taarifa za yanayoendelea kwenye kesi ya uongo dhidi ya Mwenyekiti Mbowe. Haki lazima ifanyike na ionekane imefanyika. Haki haiwezi kufanyika gizani na ikaonekana imefanyika,” ameandika Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu lissu.
Baada ya mvutano kuwa mkubwa, polisi wamewaruhusu waandishi wa habari 10 kuingia na baadhi ya ndugu wa watuhumiwa. Hata hivyo walioingia mahakamani humo wametakiwa kuacha simu zao nje. Mashahidi wanaotakiwa kutoa ushahidi wao leo ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai.