ATCL yaomba radhi wateja wake kutokana na usumbufu unaojitokeza kwa wasafiri

Shirika la Ndege la Tanzania, ATCL limeomba radhi kwa usumbufu unaoendelea kujitokeza kwa wateja wao kutokana na upungufu wa ndege za shirika hilo 

Taarifa iliyotolewa na shirika hilo kupitia ukurasa wao wa mtandao wa Twitter shirika hilo limesema juhudi zinaendelea kufanyika ili kurudisha huduma kama ilivyokuwa hapo awali huku likijulisha kuwa ndege moja ya Airbus ipo katika hatua za mwisho za marekebisho na inategemewa kurudi katika miruko ya kawaida kuanzia wiki ijayo.

Siku za hivi karibuni ATCL ilitoa taarifa juu ya kupunguza miruko ya ndege zake kutokana na kufanyiwa matengenezo

“Tunaomba radhi kwa usumbufu unaoendelea kutokea kwa wateja wetu kutokana na upungufu wa ndege zetu kama tulivyowajulisha siku zilizopita”

Aidha, ATCL imesema wakati huo huo juhudi zinafanyika ili kupata ndege ya ziada kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko katika kipindi hiki cha mwaka chenye uhitaji mkubwa.

“Juhudu zinafanyika ili kurudisha huduma zetu kama awali.Pamoja na hayo tunapenda kuwajulisha kwamba ndege yetu ya Airbus ipo katika hatua za mwisho za marekebisho na inategemewa kurudi katika miruko ya kawaida kuanzia  wiki ijayo na wakati huohuo juhudi zinafanyika kupata ndege za ziada kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko katika kipindi hiki cha mwaka chenye uhitaji mkubwa”- ilisema taarifa hiyo

Hata hivyo, ATCL imeendelea kuomba radhi kwa usumbufu unaoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya ratiba, ili kuhakikisha safari zao zinafanyika pamoja na changamoto zilizopo.