Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wanachama wa chama hicho kujiandaa kukosolewa na vyama vya upinzani kwenye mikutano ya hadhara huku akiwataka wajibu hoja badala ya “kupayuka” majukwaani.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatatu Januari 10, 2022 huko Unguja, visiwani Zanzibar wakati wa kilele cha matembezi ya vijana kuadhimisha miaka 59 ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar zilizoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM),ambapo yeye akiwa mgeni rasmi.
Amesema CCM imekuja na mwelekeo wa maridhiano, ustahimilivu, mabadiliko na kuijenga upya nchi hii, kazi hiyo inatakiwa kufanyika hata kwenye chama.
Amewataka makada wa chama hicho kwenda kutumia vema fursa ya mikutano ya hadhara kwa kujibu hoja, msibwabwaje.
“Sisi kama CCM tunajipanga, kuna vyama havijipangi hivyo, watakuja na ya kwao. Watakuja kutu-challenge, watakuja kutukosoa.
“Naomba sana, tunapokosolewa tuangalie, yale ya kweli tuyachukue tuyafanyie kazi, yawe makosa yameondoka. Yale ambayo si ya kweli, twendeni tukajibu kwa hoja lakini kubwa ni utahimilivu.
“Usipokuwa mstahimilivu, utapandishwa kwenye jukwaa ukajibu hoja, hutajibu hoja, utapayuka sawa sawa na yule aliyekutia ufunguo ukapanda. Kwahiyo niwaombe sana vijana wa Chama cha Mapinduzi, tujipange,” amesisitiza Rais Samia.
Amesema pale wanapokosolewa, wafanye mabadiliko ndani ya chama, wasifanye kazi kwa mazoea.
Ameongeza kwamba watakapokwenda kupayuka, hapo hawaonyeshi uongozi kwa vyama vingine vya siasa.
“Niwaombe sana, twendeni tukafanye mabadiliko ndani ya chama, ndani ya jumuiya zetu. Yale tuliyoyazoea, ugomvi kati yetu uachwe, ukome.
“Tunakwenda kwenye mapambano ya kisiasa, tunakwenda kutetea nafasi yetu ndani ya nchi hii, tunakwenda kuonyesha kwamba sisi ni chama kiongozi,” amesema Rais Samia.
Kiongozi huyo amesema mwaka 2024 kuna uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao ni uchaguzi muhimu kwa chama chake, hivyo ameonya kwamba wakienda wamegawanyika, hawatafanya vizuri, amesisitiza waende wakiwa wamoja.
“Zama za ugomvi, kupigana na kutukanana katika siasa sasa ziishe, twendeni na hoja za maana, twendeni na hoja za kujenga. Tuvumiliane tulete maendeleo ya kweli na yenye tija ili tujenge Tanzania mpya yenye maendeleo endelevu,” amesema.