Nyuki wakatisha uhai wa mwalimu mkoani Kigoma.

Mwalimu wa shule ya msingi Mambo, iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, Deogratius Ndokoye (51) amefariki dunia mara baada ya kushambuliwa na kundi la nyuki waliokuwa katika mti wa mwembe uliopo karibu na nyumbani kwake.

Tukio hilo limetokea Februari 13, 2023  katika eneo la mtaa wa Mwasenga, Manispaa ya Kigoma Ujiji, muda mfupi mara baada ya watoto waliokuwa wakitoka shule kurusha mawe juu ya mwembe huo na kusababisha nyuki kuzagaa na kumvamia mwalimu huyo na kumshambulia na hatimaye kupoteza maisha.

Akizungumza leo Februari 15 mkoani hapa, Mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Kigoma Maweni, Stanley Binagi amesema walimpokea Ndokoye akiwa ameshafariki na huku mwili wake ukiwa umevimba hadi kichwani na wenye majeraha.

Binagi amesema na mara baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wake waligundua kilichopelekea kifo chake ni mshtuko uliosababishwa na kung’atwa na nyuki hao katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Amesema majeraha ya moto yaliyokuwa kwenye mwili wa marehemu yalitokana na mchakato wa awali wa kumuokoa maisha yake wakati wanawavukuza wadudu hao na kuwapelekea kutumia moto hivyo kusababisha majeraha mwilini mwake.

“Majeraha ya moto hayatoshi kusema kuwa yalipelekea kifo chake na pia michubuko aliyokuwa amepata mwilini mwake haitoshi kusema ndio yamepelekea kifo chake lakini mshtuko wa mwili na sumu iliyokuwa imempata baada ya kuumwa na wadudu hao ndio ilipelekea kifo chake,” amesema Binagi.

Kwa upande wake Mwenyekiti mstaafu wa kitongoji cha Masanga, Lubabi Nyabakali amesema tukio hilo sio la kwanza katika eneo hilo, kwani mara ya kwanza nyuki hao walivamia mifugo ambapo mbwa wawili walikufa.

Ameziomba mamlaka za maliasili kufanya harakati za kuwatoa nyuki hao na ikibidi mwembe huo ukatwe kwa ajili ya usalama wa wananchi.

Baadhi ya majirani wamesema walifanya jitihada za kuyaokoa maisha yake lakini hawakufanikiwa kutokana na nyuki hao kuwa wengi na kushindwa namna ya kuwadhibiti kwa uharaka.