Ofisi ya Askofu Jimbo Katoliki la Geita imeazimia kusitisha huduma zote za kiibada na kisakramenti katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo Katoliki la Geita kwa muda wa siku 20 kuanzia Februari 27 hadi Machi 18, 2023.
Uamuzi huo umetolewa leo na kupitia waraka wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Flavian Kassala, ikiwa ni siku mbili tangu kutokea kwa uvamizi na uharibifu ndani ya kanisa hilo, lililopo Mtaa wa Jimboni, Kata ya Buhalahala mjini Geita.
Amesema, hatua hiyo imekuja kwa sababu uhalifu uliofanyika ni kufuru kubwa kwa sakramenti ya ekaristi takatifu na umeivunjia sakramenti ya ekaristi takatifu heshima yake kwa kiasi kikubwa na umelinajisi kanisa.
“Kutokana na matukio hayo, kanisa hili limepoteza kwa kiasi kikubwa baraka yake na jamii ya waamini imeumizwa sana kutokana na kashfa, kufuru na unajisi uliofanyika kwa imani yetu,” ameeleza.
“Kanisa Kuu la Jimbo litafunguliwa Machi 18, 2023 kwa maadhimisho ya ibada ya misa takatifu itakayoanza saa nne asubuhi, na itakayohusisha pia maadhimisho ya toba ya malipizi, baraka ya kutakatifuza kanisa kuu na kurudisha ekaristi takatifu ndani ya kanisa,” amesema.