Waandishi wa habari 272 walipata madhila katika kipindi cha miaka 10 nchini Tanzania

Waandishi wa habari 272, kati yake wanaume 219 na wanawake 53 walikumbwa na madhila mbali mbali katika kipindi cha miaka 10 nchini Tanzania

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Kajubi Mukajanga katika kongamano la miaka 30 ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yenye kauli mbiu ‘Uhuru wa Kujieleza kama Kichocheo cha Haki Nyingine za Binadamu’ kitaifa maadhimisho hayo yanafanyika visiwani Zanzibar.

Amesema, katika kipindi hicho  cha miaka 10 toka 2013 hadi 2022, vyombo vya habari 94 vilikumbwa na madhila hayo.Matamshi au vitendo  19 vilielekezwa kwa waandishi na vyombo vya Habari kwa ujumla.

Amesema, madhila ambayo yamerekodiwa katika kanzidata ya MCT katika kipindi hicho ni 271, ambapo kukamatwa kwa waandishi wa habari wakiwa kazini, kuliongoza kwa kuwa matukio 52, ikifuatiwa na vitisho kutoka kwa watoa taarifa mbali mbali matukio 50 na waandishi wa habari kunyimwa taarifa matukio 45.

Madhila mengine ni mashambulio ya mwili, matukio 25, kufungiwa vyombo vya habari (29), faini (14), kuondolewa katika eneo la kazi au eneo la tukio kwa nguvu au kwa vitisho (10), kutekwa waandishi wa habari au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha matukio sita, kudhalilishwa matukio 13, na kujidhibiti kwa chombo cha habari matukio manne.

Pia kuna matukio 15 ya waandishi wa habari kuharibiwa na kutaifishwa vifaa vyao vya kazi, huku uminywaji wa mitandao ya kijamii matukio matatu, mauaji matukio matatu, na kuingilia uhuru wa uhariri matukio mawili.

Kajubi amesema, Kanzidata inaonyesha kuwa taasisi iliyoongoza kwa matukio mengi dhidi ya  uhuru wa habari ilikuwa ni polisi ambayo ilikuwa na matukio 51.

Wahusika wengine ni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) matukio 21, wizara mbali mbali matukio 14, wakuu wa wilaya matukio tisa, mashabiki wa mpira matukio matano, wakulima na wafugaji  matukio mawili na watu wasiojulikana matukio kumi. Idara ya Habari Maelezo (Bara) haikubaki nyuma nayo ilikuwa na matukio nane na wakuu wa mikoa matukio saba.

Wahusika wengine wa madhila yaliyowapata waandishi wa habari katika kipindi hicho ni mgambo, madiwani na watendaji kata matukio manne, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) matukio matatu, Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) matukio matatu, mahakama matukio matatu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), matukio mawili, Chama cha Mapinduzi (CCM) tukio moja, Tume ya Utangazaji Zanzibar matukio mawili, maafisa maendeleo ya jamii matukio mawili na Mwananchi Communications Limited matukio mawili.

“Wahusika wafuatao wamefungana kwa kuwa na tukio moja moja, nao ni viongozi wa dini, Azam Media Group, wapiga kura wa Msikiti wa Makanyagio, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.”

Amesema, katika mikoa 26 ya Tanzania Bara madhila kwa uhuru wa habari yaliyorekodiwa yalitokea katika mikoa 25.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa katika kipindi hicho cha miaka kumi, mkoa wa Songwe haukuwa na madhila.

Ametaja mikoa 10 ya Tanzania Bara iliyoongoza kwa madhila na idadi yake. Mkoa wenye matukio mengi zaidi ni Dar es Salaam matukio 43, Shinyanga (18), Arusha (17), Dodoma (15), Mara (13), Kagera (12), Kilimanjaro (11), Tanga (10), Ruvuma na Singida matukio nane kila mmoja; na Mwanza, Rukwa na Pwani matukio saba kila mmoja. Kwa upande wa Zanzibar (Unguja na Pemba), jumla ya madhila 15 yaliripotiwa katika kipindi hicho.

Taarifa ya idadi ya madhila iko kama ifuatavyo 2013 (38), 2014 (27), 2015 (20), 2016 (32), 2017 (5), 2018 (24), 2019 (40), 2020 (41), 2021 (26) na 2022 (18).

“Kutokea kwa madhila kumeendelea kujenga hofu miongoni mwa waandishi wa habari na vyombo vya habari na kusababisha uandishi wa habari usio wa kina  na kukosekana kwa habari za kiuchunguzi.

“Matukio haya pia yameendelea kuishusha Tanzania katika sura ya kimataifa. Kwa mfano, katika ripoti za World Press Freedom Index, Tanzania imeendelea kushuka katika viwango vya uhuru wa habari kutoka nafasi ya 70 mwaka 2013 mpaka nafasi ya 124 mwaka 2021 na mwaka 2022 nafasi ya 123.

Aidha, amesema MCT inawahimiza waandishi wa habari kufanya kazi kwa uhuru, weledi na kufuata maadili, na pale kunapokuwa na changamoto kuwasiliana na Baraza.

“Madhila kwa waandishi wa habari yasichukuliwe kama ni ‘ajali kazini’, bali ni mambo yanayotakiwa kuripotiwa na kurekodiwa ili Tanzania iwe na rekodi ya madhila ambayo waandishi wanakutana nayo”

Amesema, uwepo wa taarifa utasaidia kuonyesha ukubwa wa tatizo na kuongezwa kwa jitihada za kutafuta suluhu.