CCM yataka maoni chanya ya wananchi kuhusu mkataba wa bandari yasikilizwe.

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeielekeza Serikali kuhakikisha inasikiliza maoni chanya na yenye tija yanayotolewa na wananchi kuhusu makubaliano ya uwekezaji na uendelezaji wa bandari kati ya Tanzania na Dubai.

Wito huo umetolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) katika kikao chake cha kawaida chini ya Mwenyekiti wake Rais Samia Suluhu Hassan kilichofanyika Julai 09, jijini Dodoma.

Aidha, katika kikao hicho halmashauri imeazimia Serikali kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari pamoja na kukubaliana kuwa uwekezaji na uendeshaji huo ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi.

Kumekuwa na mjadala mzito unaendelea nchini Tanzania kwa zaidi ya wiki tatu sasa kuhusu mkataba huo ambapo mjadala mkubwa umetaja hofu iliyopo juu ya makubaliano hayo ambao yanatajwa kwenda kuiuza bandari ya Tanzania.

Baadhi ya wakosoaji wakiwemo wanasiasa wa vyama vya upinzani wameitaka Serikali kuurudia tena mkataba huo na kisha kurudishwa kwa wananchi ili kila mmoja awe na maoni huru juu ya kuboresha.

Hata hivyo wengine wamejikuta matatani baada ya kupata vitsho vya kutaka kitolewa uhai wao mara tu baada ya kujadili na kutoa maoni yao kuhusu mktaba huo.

Miongoni mwa wanaodai kutishiwa kuuawa ni aliyekuwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tangayika Law Society  Dkt. Rugemeleza Nshala ambaye hivi alitoa madai hayo kwa wanahabari kwamba habari kutoka katika vyanzo vya kuaminika vimemuarifu kuwa anatakiwa kuuawa. 

Kufuatia hayo jana Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC kimewataka baadhi ya watu waliolalamika kutishiwa maisha yao na watu wanaodai wasiojulikana kutokana na kutoa maoni katika masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya taifa, kutoa taarifa Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika hao.

“Sambamba na hilo, kumekuwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa Serikali hususani mawaziri kutoa maonyo ambayo yanaashiria kuwatishia Watanzania wanaotekeleza uhuru wao wa kutoa maoni kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, vitendo vinavyoashiria kuanza kushuka kwa uhuru wa kujieleza hapa nchini,” imesema LHRC.

Mbali na hayo imetoa wito kwa Watanzania kutumia uhuru wao wa kujieleza kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi bila kutweza utu wa mtu mwingine kwa vigezo vya jinsia, udini, ukabila, hadhi, ulemavu au rangi ya mtu