Jeshi la Polisi Tanzania limepiga marufuku maandamano yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) yenye lengo la kuunga mkono uwekezaji katika bandari.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa UVCCM, Mohammed Kawaida kupitia vyombo vya habari alitoa taarifa ya kuhamasisha maandamano ya kuunga mkono Serikali katika uwekezaji wa bandari yaliyotarajiwa kufanyika Wilaya zote kuanzia Julai 18 mwaka huu.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na msemaji wa Jeshi hilo, David Misime jana Jumapili Julai 16, 2023 imesema maandamano hayo ya nchi nzima yatazua taharuki zisizo na msingi na badala yake hoja zote ziwasilishwe katika vyombo husika.
“Kwa msingi huo, Jeshi la Polisi linapiga marufuku maandamano hayo yasifanyike na hii ni pamoja na watu wengine wenye nia kama hizo na badala yake wawasilishe hoja zao kupitia mikutano na vyombo vya habari,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Misime.
Aidha, Jeshi la Polisi limeongeza kuwa miongozo ya mtu au kikundi cha watu kinapotaka kuitisha maandamano ipo na inapaswa kufuatwa.
“Pamoja na utaratibu huo wa kisheria, kuitisha maandamano nchi nzima ni sawa na kutaka kuleta vurugu na hofu kwa Watanzania bila sababu yoyote kwani majukwaa ya kuwasilisha hoja hizo yapo,” imesema taarifa hiyo.