Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Mgomo wa Wafanyabiashara Tanzania ngoma bado nzito - Mwanzo TV

Mgomo wa Wafanyabiashara Tanzania ngoma bado nzito

Wakati wafanyabiashara katika mikoa ya Mbeya, Dodoma, Arusha  na Mwanza wakiendelea na mgomo waliouanza jana, mkoani Iringa, Geita na Mtwara nako wamegoma.

Mgomo wa wafanyabiashara hao wa maduka jijini Mbeya, Dodoma,Arusha na Mwanza ulianza jana Juni 25, unalenga kuishinikiza Serikali kuondoa utitiri wa kodi na tozo mbalimbali ambazo si rafiki kwa wafanyabiashara.

Huu ni mwendelezo wa kilichofanywa na wafanyabiashara wenzao katika soko la Kariakoo jijini Dar es salaam ambao walianza mgomo siku ya Jumatatu Juni 24,2024 na leo mgomo huo ukiingia siku ya tatu.

Hata hivyo,  wafanyabiashara ndogo ndogo ‘mamchinga’ wanaendelea kuuza bidhaa zao.

Mkoani Iringa

Wafanyabiashara Mkoa wa Iringa wameungana na wenzao kufunga maduka wakiishinika Serikali kusikiliza malalamiko yao dhidi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Baadhi ya wanunuzi wamelalamikia hali hiyo na kuiomba Serikali iingilie kati kumaliza mgomo huo.

Hali ilivyo Jijini Mwanza

Wakati Polisi wakitapakaa mitaani Jijini Mwanza, wafanyabiashara wao wanaendelea na mgomo wao waliouanza jana Jumanne Juni 25, 2024.

Wapo maofisa wa Jeshi la Polisi wanaotembea na waliopo kwenye magari, wakipita katika mitaa mbalimbali ya jijini hilo, huku maduka yakiwa yamefungwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amethibitisha kuwasambaza askarimitaani, huku akidokeza kuwa jukumu lao ni kuimarisha ulinzi kwa wafanyabiashara watakaofungua maduka wasifanyiwe fujo na waliogoma.

Kamanda Mutafungwa amesema ulinzi na doria hizo zitakuwa endelevu hadi hali itakaporejea katika utimamu na kuwaonya watakaojaribu kuwafanyia vurugu wafanyabiashara walioridhia kufungua maduka yao.

Hali hiyohiyo ndio inayoendelea katika mikoa ya Geita, Mtwara, Dodoma na Arusha.

Wafanyabiashara wanaitaka Serikali kupunguza kodi, kuwawekea mazingira mazuri ya biashara lakini pia kuwekwa kwa mifumo mizuri ya ukusanyaji kodi tofauti na inavyofanywa hivi sasa.

Wakati mgomo huu ukiendelea tayari viongozi wa Serikali nchini wamewataka wafanyabishara kufungua maduka kote nchini huku mazungumzo yakiendelea.

Hata hivyo wafanyabiashara wameonekana kukaidi agizo hilo.

Hii leo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikutana na Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania kwa ajili ya mazungumzo

Juni 24, 2024 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwa niaba ya Serikali wakati akitoa maazimio ya kikao kati ya viongozi wa wafanyabiashara Tanzania, viongozi wa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo na taasisi zinazosimamia masuala ya wafanyabiashara na kuweka maazimio yaliyotajwa kuwa yanakwenda kubadilisha mifumo ya biashara inayolalamikiwa na wafanyabiashara.

Miongoni mwa maazimio hayo ni kwamba Serikali imesitisha kazi ya ukaguzi wa risiti za kielektroniki (EFD) na ritani za kodi  iliyokuwa ikifanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia mkoa wa kikodi wa Kariakoo, jijini  Dar es Salaam, wakati ukiandaliwa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo katika Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo.

‘’Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo awaomba wafanyabiashara kufungua maduka’’

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Soko la Kimataifa la Kariakoo Martin Mbwana ametoa rai kwa wafanyabiashara kufungua maduka yao na kuendelea kufanyakazi zao wakati serikali ikiendelea na mchakato wa kutatua madai yao.

Rai hiyo ameitoa leo juni 26,2024 sokoni hapo wakati akiongea na wafanyabiashara wa soko hilo kuhusu maazimio waliyoyafikia na serikali katika kikao chao kilichofanyika Dodoma.

Amesema serikali imeahidi kushughulikia changamoto zao ambapo kwa kuanza TRA imeridhia kutokufika katika soko hilo na kukamata kamata mpaka hapo watakaposhughulikia mifumo yao.

Amesema pamoja na TRA kusitisha kamatakamata pia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewataka TRA kuboresha mfumo wa forodha bandarini ambapo mpaka kufikia Agosti 8 mfumo uwe umesharekebishwa.

“Nikiwa kama muwakilishi wenu wafanyabiashara niwaombe mfungue biashara zenu kwa hiyari muendelee kufanyabiashara kwani serikali imeridhia madai yetu na imeahidi kushughulikia hatulazumishi mtu kufungua maana kufunga na kufungua ni utashi wa mtu mwenyewe”,Amesema Mbwana.

Sambamba na hayo Mwenyekiti huyo amewataka polisi kutokutumia nguvu kwa wafanyabiashara kwani kufunga na kufungua ni wajibu wa mfanyabiashara mwenyewe.

‘Wafanyabiashara wagoma’

Kutokana na kauli hiyo ya mwenyekiti, baadhi ya wafanyabiashara wameonekana kutoridhishwa na kile kilichozungumzwa, huku wakisema kilichoelezwa ni kimoja wakati wana changamoto zaidi ya hiyo.

Wamesema  walitegemea kiongozi wao atakuja na majibu ya kuwaridhisha, ili wafungue maduka lakini kwa kiasi kikubwa ameongea kisiasa.

Kinachoonekana kwa sasa kama wafanyabiashara kuna watu wanawashinikiza kufunga maduka, jambo ambalo halina ukweli.

Hii si mara ya kwanza kwa Wafanyabiashara kufanya migomo nchini Tanzania, na katika awamu zote za migomo hiyo malalamiko mara zote yamekuwa ni yale yale.

Mei 17, mwaka 2023, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliunda kamati ya watu 14 ikiwa ni saba kutoka serikalini na saba Jumuiya ya Wafanyabiashara kwa ajili ya kushughulikia kero za kundi hilo na kupendekeza hatua stahiki za kuchukuliwa.

Hatua hiyo ilikuja baada ya wafanyabiashara kugoma kufungua biashara kwa siku kadhaa, hali iliyolazimu Waziri Mkuu akiwa ameambatana na mawaziri kwenda kuzungumza nao kwa kusikiliza kero za mmoja mmoja.

Hata hivyo, ripoti ya kamati hiyo haijawahi kuwekwa hadharani.