Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Lissu ambaye pia ni Mgombea Uenyekiti wa Chama hicho, amefika Ofisi za Makao Makuu ya Chadema zilizopo Mikocheni jijini Dar es salaam na kuchukua rasmi fomu ya kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza na Wanahabari mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea, Tundu Lissu amesema kuwa anaamini hatua hiyo itakuwa ni mwanzo mpya wa mabadiliko ya kweli ndani ya Chadema na kwa Taifa kwa ujumla ambapo anatarajiwa kuirudisha fomu hiyo mapema hapo kesho.
“Siku ya leo ni siku ya kufungua ukurasa mpya katika historia ya chama chetu, ni siku ya kufungua ukurasa mpya kwa sababu ambazo nilizozielezea kwa kirefu siku ya Ijumaa iliyopita kwa kuilelezea kwenu na kuandika ule waraka wa kwanini ninagomeba.Katibu Mkuu amenikabidhi fomu za kugombea, naenda kuzijaza hizi fomu kama inavyotakiwa na kesho tukijaaliwa nitazirudisha na kuzikabidhi kwa Katibu Mkuu baada ya kulipia malipo ya fomu yanayostahili, jana Katibu Mkuu alisema ni shilingi 1,500,000/=” amesema Lissu mapema leo mara baada ya kuchukua fomu.
Kadhalika Lissu ameweka wazi juu ya aliyetoa fedha kwa ajili yake kuchukua fomu hiyo akisema kwamba ni Edgar Edson Mwakabela maarufu kama Sativa licha ya kuwa na uwezo wa kuilipia yeye mwenyewe na wanachama wengine kumchangia
“Hizi fomu zinatakiwa zilipiwe hiyo ada yake ya shilingi 1,500,000/= ningeilipia mimi mwenyewe, kuna wanachama wema wanaofikiri kama mimi kwamba uchaguzi huu uwe mwanzo mpya kwa chama chetu, ambao wamechanga fedha kwa ajili ya kulipia hii gharama ya kuchukulia na kurudishia fomu lakini hata hivyo hiyo fedha waliochanga wanachama haitatumika kulipia hizi fomu na fedha yangu mwenyewe vilevile haitatumika kulipia hizi fomu. Hiyo shilingi 1,500,000/= inayotakiwa kulipa hizi fomu imetolewa na mwanachama wetu mmoja anayeitwa Edgar Edson Mwakabela kwa jina maarufu anaitwa SATIVA” amesema Lissu na kuongeza kuwa
“SATIVA ndiye aliyekamatwa na watu wa usalama wa nchii, akateswa, akapigwa risasi na kutupwa porini kwenye mapori ya mkoa wa Katavi, Mungu si Athuman SATIVA yuko hai leo, yuko uhamishoni imebidi akimbie Tanzania ili wasimmalizie, wasije wakamuua kama walivyokusudia na amenipigia simu akaniambia Mh. mimi naomba nikulipie hiyo fomu, na naomba nikulipie hiyo fomu kwa sababu naamini kama ukiwa Mwenyekiti wa hiki Chama utafanya ile kazi inahitajika kufanyika katika nchi hii”-
Novemba 12, 2024 Lissu ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa alitangaza kuwania nafasi hiyo ambapo katika miongoni mwa mazungumzo yake amesema kumekuwapo na ushawishi kutoka kwa wanachama wa chama hicho wakimtaka yeye awanie nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
Viongozi wengine waliowahi kushika nafasi ya Uenyekiti Taifa wa CHADEMA ni Edwin Mtei, mwanzilishi wa chama hicho, na baadaye 2002 hadi 2003 Bob Makani, ambaye alishika nafasi hiyo baada ya Mtei na Mbowe, anayeshikilia nafasi hiyo kuanzia 2004 mpaka sasa.
Hadi sasa hakuna taarifa rasmi juu ya Mwenyekiti wa sasa Freeman Mbowe iwapo atawania tena kiti hicho au laa, hata hivyo kwa mujibu wa taarifa ya Chadema hadi sasa watu watatu wametanga nia ya kugombea nafasi hiyo licha ya kwamba majina yao hayakuwekwa wazi.