Congress yathibitisha ushindi wa Donald Trump

Makamu wa Rais wa Marekani na aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Demcratic, Kamala Harris, ameongoza shughuli ya bunge la nchi hiyo kuidhinisha ushindi wa hasimu wake, Donald Trump, kuwa rais mpya.

 

Kinyume na hali ilivyokuwa miaka minne iliyopita, siku ya Jumatatu (Januari 6) bunge la Marekani lilifanikisha kwa wepesi tukio hilo ambalo ni alama ya mila ya kidemokrasia kwa taifa hilo kubwa duniani bila ya mashaka yoyote.

 


Makamu wa Rais Kamala Harris alisimamia zoezi hilo la kuhisabiwa kura za wajumbe na kisha akamtangaza rasmi aliyekuwa mpinzani wake kwenye uchaguzi wa Novemba 9 kuwa ndiye mshindi halali.

 

“Matokeo ya kura ya rais wa Marekani, kama yalivyowasilishwa kwa rais wa Baraza la Seneti ni kama ifuatavyo. Idadi kamili ya wajumbe walioteuliwa kumchagua rais wa Marekani ni 538. Ndani yake, wingi wa kura ni 270. Kura za rais ni kama ifuatavyo: Donald J. Trump wa jimbo la Florida amepata kura 312. Kamala D. Harris wa jimbo la Carlifornia amepata kura 226. Kura za makamu wa rais ni kama ifuatavyo: J.D. Vance wa jimbo la Ohio amepata kura 312. Tim Walz wa jimbo la Minnesota amepata kura 226.” Alisema makamu huyo wa rais.

 

Kabla ya kutoa tangazo hilo, Kamala Harris alikuwa ametekeleza wajibu wake huo wa kikatiba kwa kusimama kwenye ukumbi wa bunge akipitisha kila nakala ya matokeo ya uchaguzi kwa wabunge na kila karatasi ya matokeo ya kura ilipotajwa alisimama akiwa amekunja mikono yake.

 

Baadaye, makamu huyo wa rais kutokea chama cha Democrat aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwake ilikuwa siku muhimu muhimu sana kwa demokrasia ya Marekani, akiongeza kwamba “hii ndiyo mila Wamarekani wanayopaswa kuifurahikia, ambayo ni mojawapo wa misingi muhimu ya demokrasia yetu, yaani kuwa ni ukabidhianaji wa madaraka kwa njia za amani. Na leo nimetenda kile ambacho nimekuwa nikikifanya maishani mwangu mote, ambacho ni kutimiza kiapo changu cha kuilinda katiba ya Marekani.”