Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya Petroli hapa nchini zitakazotumika kuanzia leo Jumatano tarehe 05 Februari 2025 saa 6 usiku, kwa mwezi Februari 2025 bei za rejareja na jumla.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo, bei ya petroli kwa rejareja katika Jiji la Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 0.957, dizeli kwa asilimia 2.18 na mafuta ya taa kwa asilimia 1.25.
Kutokana na ongezeko hilo wanunuzi wa mafuta kwa bei ya rejareja katika Jiji la Dar es Salaam watanunua lita moja kwa Sh2, 820 kwa petroli, dizeli Sh2, 703 na mafuta ya taa kwa Sh2, 710.
Bei hizo ni kutoka Sh2, 793 kwa bei ya petroli ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa Januari mwaka huu, dizeli Sh2, 644 na mafuta ya taa kwa Sh2, 676.
Kwa mujibu wa Ewura, ongezeko hilo la bei huenda limechangiwa na kuongezeka kwa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) kwa asilimia 4.77.
“Gharama za mafuta (FOB) na gharama za uagizaji (Premiums) zinalipiwa kwa kutumia fedha za kigeni ikiwemo Dola ya Marekani. Kwa bei za mwezi Februari 2025, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umeongezeka kwa asilimia 4.77,” imesema taarifa ya Ewura.