Dkt Slaa aachiwa huru baada ya siku 48 rumande, atangaza kurudi Chadema

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es salaam imemuachilia huru Dkt. Wilbord Slaa(76) baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini DPP kueleza kuwa hana nia ya kuendelea na shauri hilo.

Shauri hilo  Na.993 la mwaka 2025 linaeleza kuwa Dkt. Slaa ameshtakiwa kwa kuchapisha taarifa za uongo kupitia ukurasa wa X (zamani Twitter). 

Leo February 27,2025, Wakili wa Serikali Mwandamizi Job Mrema amewasilisha nia ya DPP mbele ya Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga .

Wakili Mrema ameieleza Mahakama kuwa DPP ameamua kutoaendelea na shauri hilo kwa mujibu wa kifungu cha 91 (1) cha mwenendo wa makosa ya jinai.

Ikumbukwe kuwa Dkt Slaa alikamatwa Januari 10,2025 na kufikishwa Mahakama ya Kisutu , kujibu shtaka la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X (zamani twitter).

Wakili Kato, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki alidai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikielezwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi aliandika ujumbe uliosomeka:

 “Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya… na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa… hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”

Dk Slaa ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mbunge wa Karatu na Balozi wa Tanzania nchini Sweden mpaka leo hii anaachiwa huru amekaa rumande bila dhamana kwa takribani  siku 48 tangu aliposhikiliwa.

Amekuwa mkosoaji mkubwa wa Serikali hali iliyofanya kuvuliwa hadhi yake ya Ubalozi.

-Aweka wazi kurudi Chadema-

Hata hivyo mara baada ya kuachiliwa huru Dk Slaa, amekiri kusema kwamba kwa sasa yuko tayari kurudi katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kwa kile alichoeleza kwamba kilichomuondoa katika chama hicho sasa hakipo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka mahakamani, ambapo ameachiwa huru baada ya kuwekwa ndani kwa siku zaidi ya 40, Dk Slaa amesema kwa sasa hana tatizo la kufanya kazi kwa karibu zaidi na chama hicho cha upinzani.

“Mimi nadhani kwa sababu kile tunachokipigania wamekiweka wazi , sasa hivi kile kilichoniondoa 2015 kimeshafutika , sina tatizo lolote kufanya kazi kwa karibu zaidi na CHADEMA kwa utaratibu wa CHADEMA” amesema Dk.Slaa.