Katika hali inayoashiria mabadiliko ya mitazamo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), orodha ndefu ya wabunge na wanasiasa wakongwe imeshindwa kuvuka kizingiti cha kura za maoni zilizofanyika tarehe 4 Agosti 2025, katika majimbo mbalimbali ya uchaguzi nchini Tanzania.
Ingawa majina ya mwisho ya wagombea yataamuliwa na ngazi za juu za chama hicho, matokeo ya sasa yameweka uelekeo wa wazi kuwa sehemu kubwa ya wanachama wameonyesha hamu ya kuona sura mpya zikipewa nafasi ya uongozi.
Wabunge waliotemwa na wagombea wapya
Katika Jimbo la Vunjo, Dr. Charles Kimei, aliyewahi kuhudumu kama mbunge tangu mwaka 2020, ameondolewa na Enock Zadock Koola, aliyeibuka na kura 1,999 Kati ya 4080 akiwabwaga wenzie watano (5) wakiongozwa na mbunge anayemaliza muda wake Dr Charles kimei aliyepata kura 861 na kushika nafasi ya pili
Koola alishinda pia katika mchakato kama huo mwaka 2020 lakini hakuteuliwa.
Moshi Vijijini, Prof. Patrick Ndakidemi alishindwa na Moris Makoi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, aliyepata kura 2,148 dhidi ya 627 za Ndakidemi.
Katika Iringa Mjini, aliyekuwa mbunge Jesca Msambatavangu alijikuta akishika nafasi ya nne kwa kura 408. Kura nyingi zilikwenda kwa Fadhil Ngajilo (1,899), Wakili Moses (1,523) na Mchungaji Peter Msigwa (477).
Jimbo la Kyerwa limeona mabadiliko makubwa, ambapo Khalid Nsekela alipata ushindi wa kishindo kwa kura 5,693, sawa na asilimia 71, dhidi ya Innocent Bilakwate aliyepata kura 1,567.
Katika jimbo la Makambako, aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, alipata ushindi wa kushangaza kwa kura 6,151, akiwaacha mbali wenzake, wakiwemo Deo Sanga (Jah People) aliyepata kura 470 pekee – sawa na asilimia 7.1.
Tabora Mjini, aliyekuwa mbunge Emmanuel Mwakasaka alipata kura 228 pekee, nyuma ya Shabani Mrutu aliyeshinda kwa kura 6,612. Mwakasaka pia alizidiwa na wagombea wengine akiwemo Hawa Mwaifunga (326) na Kisamba Tambwe (395).
Kwa upande wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu, aliyekuwa mbunge kwa miaka 10, alipata kura 2,097 na kushindwa kwa tofauti ndogo na Chacha Wambura aliyepata kura 2,145. Upendo Peneza alipata kura 1,272 huku wengine wakipata kura za chini.
Jimbo jipya la Katoro limempa ushindi Kija Ntemi kwa kura 2,134, akifuatiwa kwa karibu na Ester James (2,075), huku Tumaini Magesa, aliyekuwa mbunge wa Busanda, akishika nafasi ya tatu kwa kura 1,265.
Namtumbo ilishuhudia Dkt. Juma Zuberi Homera, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, akiongoza kwa kura 11,836 (asilimia 92), dhidi ya aliyekuwa mbunge Vita Kawawa, aliyepata kura 852 tu.
Mtwara Mjini, Joel Arthur Nanauka alitangazwa mshindi kwa kura 2,045, akimshinda Hassan Mtenga, mbunge anayemaliza muda wake, aliyepata kura 1,607.
Lindi Mjini, Mohamed Utali alipata kura 1,474 kati ya 3,289 zilizopigwa, na kumbwaga mbunge wa sasa Hamida Abdalla, aliyepata kura 876.
Nyasa, aliyekuwa Naibu Waziri na mbunge mkongwe Stella Manyanya, alipata kura 548 tu, huku John Nchimbi akipata kura 9,157 kati ya 10,695.
Jimbo la Muleba Kaskazini limeandika sura mpya, baada ya Adonis Bitegeko kumshinda aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Mbunge wa muda mrefu, Dkt. Charles Mwijage.
Sauti ya Wajumbe au maamuzi ya juu?
Kwa sasa, macho na masikio yameelekezwa kwenye makao makuu ya CCM, ambako vikao vya juu vinatarajiwa kupitia na kupitisha au kubadili matokeo ya kura za maoni. Wanachama wengi wanataka kuona iwapo sauti yao itaheshimiwa, au kama baadhi ya waliokataliwa watarejeshwa kwa misingi ya uzoefu wa kisiasa.
Kwa waliokataliwa, matumaini yaliyosalia ni msamaha wa kisiasa kutoka juu. Lakini ujumbe kutoka mashinani ni wazi wito wa mabadiliko umeenea, na wanachama wanataka damu mpya.