Amnesty yalaani ukiukaji wa haki za binadamu wa “kitaasisi” nchini Tanzania

Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu, Amnesty International, jana Jumatatu lililaumu kile ilichokiita “ukiukaji wa haki za binadamu wa kitaasisi” unaofanywa na mamlaka nchini Tanzania, ukiwa unaongezeka kadri uchaguzi wa urais unavyokaribia, uchaguzi ambao unawaondoa wagombea wa upinzani.

Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan, ambaye awali alisifiwa kwa kulegeza masharti makali yaliyowekwa na mtangulizi wake mwenye utawala wa kiimla, John Magufuli, sasa anakabiliwa na ukosoaji mkali kutoka kwa vyama vya upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali anapotafuta kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Oktoba 29.

Kati ya Januari 2024 na Oktoba 2025, Amnesty iliripoti ukiukaji mpana wa haki za binadamu ikiwemo matukio ya watu kupotea kusikojulikana,  mateso na mauaji ya kiholela ya viongozi na wanaharakati wa upinzani.

Ripoti hiyo ya Amnesty, ilitokana na mahojiano na watu 43 wakiwemo mashahidi, waathirika, ndugu wa waathirika, wanachama wa mashirika ya kiraia na mawakili, pamoja na uchambuzi wa picha na machapisho mbalimbali.

Mnamo Septemba 2024, Ali Mohamed Kibao, kiongozi mwandamizi wa chama kikuu cha upinzani Chadema mwenye umri wa miaka 69, alitekwa nyara na baadaye kupatikana akiwa ameuawa. Uchunguzi ulianzishwa kuhusu mauaji hayo ya kikatili, lakini hadi sasa hakuna maendeleo yaliyotangazwa, Amnesty ililalamika.

Aidha, Humphrey Hesron Polepole, aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba na ambaye pia alikuwa mkosoaji wa serikali, alipotea mwezi huu.

Kwa mujibu wa Tigere Chagutah, mkurugenzi wa kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Amnesty, mamlaka za Tanzania “zimeongeza ukandamizaji wa nafasi ya kiraia na haki ya kushiriki kwa uhuru katika uchaguzi kupitia kupitisha sheria zenye mapungufu makubwa.”

Chama cha Chadema kimetengwa kushiriki uchaguzi huo kwa kukataa kusaini Kanuni za Maadili ya Uchaguzi.

Kiongozi wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye alikamatwa Aprili, anashtakiwa kwa uhaini, kosa linaloweza kuadhibiwa kwa kifo.

Wakati huo huo, Luhaga Mpina, mgombea wa chama cha tatu kwa ukubwa, Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), amezuiwa kugombea.