Marekani yarejesha msaada wa chakula Somalia

Marekani imetangaza kurejesha usambazaji wa msaada wa chakula nchini Somalia, wiki chache baada ya ghala la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lililofadhiliwa na Marekani kuharibiwa katika bandari ya Mogadishu.

Mwanzoni mwa Januari, Washington ilisimamisha msaada huo kwa Somalia kufuatia taarifa za wizi na kuingiliwa kwa shughuli za misaada na Serikali ya Somalia. Marekani ilidai kuwa maofisa wa Somalia walikamata kinyume cha sheria tani 76 za chakula cha msaada kilichokuwa kimetolewa kwa ajili ya raia waliokuwa katika mazingira magumu.

Baada ya hatua hiyo, maofisa wa Marekani walionya kuwa kurejeshwa kwa msaada wowote kungetegemea hatua za uwajibikaji zitakazochukuliwa na Serikali ya Somalia. Hata hivyo, Serikali ya Somalia ilijibu kwa kusema kuwa kubomolewa kwa ghala hilo kulikuwa sehemu ya kazi za upanuzi na maboresho ya bandari ya Mogadishu.

Jumatano, Serikali ya Somalia ilitangaza kuwa bidhaa zote za WFP zilizoathiriwa na upanuzi wa bandari zimerejeshwa. Katika taarifa yake, serikali hiyo ilisema inachukua dhamana kamili ya tukio hilo na imeipatia WFP ghala kubwa zaidi na linalofaa ndani ya eneo la bandari ya Mogadishu.

Kwa upande wake, Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema kupitia ujumbe uliowekwa kwenye mtandao wa X kuwa itarejesha usambazaji wa chakula cha WFP huku ikiendelea kutathmini upya mwelekeo wa msaada wake kwa Somalia.

“Tawala ya Rais Trump ina sera kali ya kutovumilia kabisa upotevu, wizi au matumizi mabaya ya rasilimali za Marekani,” ilisema taarifa hiyo.

Rais wa Marekani Donald Trump amekuwa akipunguza misaada ya kimataifa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita. Wakati huo huo, raia wa Somalia wanaoishi Marekani wamekuwa miongoni mwa waliolengwa katika oparesheni za ukaguzi wa uhamiaji katika wiki za hivi karibuni.

Aidha, baadhi yao wamekuwa wakituhumiwa kuhusika katika udanganyifu mkubwa wa mifumo ya misaada ya kijamii katika jimbo la Minnesota, ambalo lina jamii kubwa zaidi ya Wasomali nchini Marekani, ikikadiriwa kuwa na takribani watu 80,000.