Tanzania yatetea mpango wa uhamaji wa hiari Ngorongoro mbele ya UNESCO

Serikali ya Tanzania imeutetea mpango wa uhamaji wa hiari wa wakazi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro mbele ya Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO, ikisema hatua hiyo inalenga kulinda haki za binadamu, kuhifadhi utu wa wananchi na wakati huo huo kuhakikisha uendelevu wa uhifadhi wa eneo hilo.

Kauli hiyo imetolewa katika kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia kinachoendelea jijini Busan, ambapo Tanzania imewasilisha matokeo ya tathmini iliyofanywa na Tume ya Rais kuhusu changamoto zinazolikabili Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, ikiwemo ongezeko la watu, matumizi ya ardhi na athari zake kwa shughuli za uhifadhi.

Akiwasilisha taarifa hiyo, Katibu wa Tume ya Rais iliyochunguza masuala ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro, Thadei Kabonge, amesema tathmini hiyo ilifanyika kwa kipindi cha miezi saba baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuunda Tume mbili kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya wanajamii wa Kimasai kuhusu hali ya maisha na matumizi ya ardhi katika eneo hilo.

Kabonge amesema matokeo ya tathmini yanaonyesha kuwa idadi ya watu ndani ya eneo la hifadhi imeongezeka kwa kasi, kutoka takribani watu 8,000 mwaka 1959 hadi 100,793 mwaka 2022. Aidha, makadirio yanaonyesha kuwa idadi hiyo inaweza kufikia watu 276,651 ifikapo mwaka 2050 ikiwa hakutakuwa na hatua za kudhibiti ongezeko hilo.

Kwa mujibu wa tathmini hiyo, ongezeko la watu limeambatana na kuongezeka kwa mahitaji ya ardhi, hali iliyochochea ushindani kati ya shughuli za uhifadhi wa mazingira, utalii na maendeleo ya jamii zinazotegemea eneo hilo.

Mbali na ongezeko la watu, Tume imebaini kuwa idadi ya mifugo imeongezeka kutoka 261,723 mwaka 1960 hadi 715,466 mwaka 2022, huku idadi ya makazi ikiongezeka kutoka nyumba 13,381 mwaka 2019 hadi 17,734 mwaka 2025.

Kabonge amesema hali hiyo imeongeza shinikizo katika maeneo ya malisho na njia zinazotumiwa na wanyamapori kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine, jambo ambalo limeendelea kuathiri malengo ya uhifadhi na pia maisha ya jamii zinazotegemea mifugo.

Kwa mujibu wa tathmini hiyo, uwezo wa kaya kujikimu kupitia ufugaji umeendelea kupungua. Tume imeeleza kuwa mwaka 2022 wastani wa mifugo kwa kila mtu ulikuwa TLU 3.5, kiwango ambacho ni chini ya makadirio ya TLU nane yanayohitajika kwa mtu mmoja ili kufikia maisha endelevu ya ufugaji. 

Endapo mwenendo wa sasa utaendelea, kiwango hicho kinatarajiwa kushuka hadi TLU 1.5 kwa kila mtu ifikapo mwaka 2050.

Tathmini hiyo pia imeonyesha kuongezeka kwa migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika eneo hilo. Kati ya mwaka 2015 na 2025, watu 77 walipoteza maisha kutokana na mashambulizi ya wanyamapori, huku wengine 274 wakijeruhiwa na mifugo 1,450 kuuawa.

Serikali ya Tanzania imeendelea kusisitiza kuwa mpango wa uhamaji wa hiari unalenga kupunguza shinikizo katika eneo la hifadhi, kuboresha ustawi wa wananchi na kuhakikisha Ngorongoro inaendelea kuhifadhi hadhi yake kama moja ya maeneo ya Urithi wa Dunia wa UNESCO, huku haki za wakazi zikizingatiwa katika utekelezaji wa mpango huo.

Hata hivyo, suala la uhamaji wa wakazi kutoka Ngorongoro limeendelea kuzua mjadala ndani na nje ya Tanzania, ambapo baadhi ya makundi ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakitaka mchakato huo ufanyike kwa uwazi, kwa ridhaa ya wananchi na kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya haki za binadamu. 

Serikali kwa upande wake imeendelea kusisitiza kuwa uhamaji huo ni wa hiari na unalenga kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto za uhifadhi na maendeleo ya wananchi.