Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa ghasia na ukiukaji wa sheria katika matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Tume hiyo imepewa jukumu la kuchunguza kwa kina watu waliohusika katika ghasia hizo, ikiwa ni pamoja na kubaini waliochochea matukio hayo na waliotoa fedha au rasilimali zilizowezesha kutokea kwa ghasia.
Akizindua tume hiyo jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema uamuzi huo unatokana na mapendekezo ya tume iliyopita iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman.
Tume hiyo ya awali iliwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Aprili 23, 2026, ikipendekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina zaidi ili kubaini wahusika wa ghasia na kuwezesha hatua za uwajibikaji kuchukuliwa.
Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026, tume hiyo ilisema watu 518 walifariki, huku wengine 2,390 wakijeruhiwa kutokana na matukio hayo. Kati ya waliofariki, 21 walikuwa watoto na 16 walikuwa maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Tume hiyo pia ilibaini kuwa sehemu kubwa ya vifo hivyo vilitokana na majeraha ya risasi. Kwa mujibu wa uchambuzi wa miili iliyofanyiwa uchunguzi wa kitaalamu, vifo 197, sawa na asilimia 90, vilihusishwa na kupigwa risasi.
Hata hivyo, mwenyekiti wa tume hiyo alisisitiza kuwa idadi ya vifo iliyotajwa haipaswi kuchukuliwa kuwa ya mwisho kabisa, akisema huenda kukawa na majeruhi waliotibiwa nje ya mfumo rasmi na baadaye kufariki, pamoja na taarifa za watu waliopotea ambazo ziliwasilishwa kwa tume.
Kutokana na ukubwa wa madhara hayo, Tume ya Jaji Chande ilipendekeza uchunguzi zaidi ufanyike ili kubaini wahusika na kuwezesha hatua za uwajibikaji kuchukuliwa. Pendekezo hilo ndilo lililozingatiwa na Rais Samia katika kuunda tume mpya inayolenga kuwabaini wahusika wa ghasia na ukiukaji wa sheria.
-Majaji kutoka Tanzania, Uganda na Namibia-
Tume mpya ina makamishna sita, akiwemo mwenyekiti wake Jaji mstaafu Shaban Ali Lila. Wajumbe wengine wanatoka Tanzania, Uganda na Namibia.
Rais Samia amesema uamuzi wa kuwashirikisha majaji kutoka Uganda na Namibia unalenga kuipa tume mtazamo mpana katika uchunguzi wake.
Miongoni mwa wajumbe hao ni Jaji Barishaki Cheborion kutoka Uganda na Jaji Petrus Tilainge Damaseb kutoka Namibia, pamoja na majaji wastaafu kutoka Tanzania.
Kwa mujibu wa Rais Samia, tume inapaswa kuchunguza kwa undani zaidi nani waliochochea ghasia, nani waliohusika na matukio hayo na nani waliotoa fedha zilizotumika katika kuyawezesha.
“Tume hii inakwenda kuingia kwa undani zaidi kutafuta nani hasa waliochochea, waliohusika na waliotoa fedha ili mambo yale yatokee ndani ya nchi yetu,” amesema Rais Samia.
-Miezi mitano ya uchunguzi-
Tume hiyo imepewa muda wa siku 150, sawa na takriban miezi mitano, kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti na mapendekezo kwa mujibu wa sheria.
Rais Samia amesema iwapo tume itaomba kuongezewa muda, serikali italitathmini ombi hilo ili kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa upana unaohitajika.
Aidha, amewataka Watanzania kutoa ushirikiano kwa tume hiyo na kuepuka kuingilia kazi yake.
Kuundwa kwa tume hiyo ni hatua ya pili ya uchunguzi kuhusu ghasia na uvunjifu wa amani uliofuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Tume ya kwanza, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, iliundwa kuchunguza matukio ya ghasia na uvunjifu wa amani yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi.
Baada ya kupokea ripoti yake, Rais Samia amesema aliamua kuunda tume mpya kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.
Tume hiyo mpya sasa inatarajiwa kulenga zaidi suala la uwajibikaji wa wahusika, kwa kubaini waliohusika moja kwa moja au kwa njia nyingine katika matukio hayo.
Rais Samia amesema anaamini wajumbe wa tume hiyo watatumia taaluma, uzoefu na viapo vyao kufanya kazi kwa weledi, umakini na uadilifu.