, ,

#BREAKING: Sifuna Avuna Ndani Ya Chama Kipya- The Equitable Party

Wadh Kassim Avatar

Katika siku za hivi karibuni, jina la Edwin Sifuna limekuwa gumzo kubwa katika siasa za upinzani nchini Kenya. Baada ya kushinda kesi ya tribunal na kupata ruhusa ya kusajili Linda Mwananchi Movement, wengi walitarajia harakati hiyo iwe alama mpya ya wananchi. Lakini kwa mshangao wa wengi, Sifuna aliamua kujiunga na The Equitable Party- TEP na Sasa anatarajiwa kuendeshwa gurumu la chama hicho kama Kiongozi mkuu na mwaniaji wa kiti ha urais 2027.

 

Linda Mwananchi Movement ilianza kuvuma mapema mwaka 2026, hasa baada ya kifo cha Raila Odinga, ambapo ODM ilikumbwa na mgongano wa urithi wa kisiasa. Katika kipindi hicho, Sifuna alijitokeza kama sauti ya kujitegemea, akijaribu kuunda harakati mpya yenye sura ya wananchi… Ndipo jina la Linda Mwananchi likaanza kushika kasi mitandaoni na kwenye mikutano ya vijana, likionekana kama ishara ya upinzani mpya usiofungwa na urithi wa ODM.

 

Sifuna alitangaza nia ya kulisajili rasmi kama chama cha kisiasa, lakini mara tu baada ya kuwasilisha maombi, Msajili wa Vyama vya Kisiasa alileta pingamizi akidai jina linafanana na chama kingine kilichokuwa kimesajiliwa awali. Hatua hii ilisababisha kesi ya tribunal, ambapo Sifuna na wafuasi wake waliibuka washindina mahakama ikaamuru jina la Linda Mwananchi lihifadhiwe kwa siku 90. Hata hivyo licha ya ushindi huo… usajili kamili haukukamilika.

 

TEP kwa upande wake si chama kipya. Kilisajiliwa rasmi mnamo Machi 25, 2022 na waanzilishi wake ni pamoja na Caroli Omondi, Eunice Juma, Kerry Karani na Dr. Gilbert Changa. Chama hiki kilibuniwa kwa kauli mbiu “Tusawazishe”, kikilenga usawa wa kijamii na kiuchumi kupunguza pengo la kiuchumi, kupambana na ufisadi na kuunganisha Wakenya kutoka makabila na vizazi tofauti.

 

Sababu kuu ya Sifuna kujiunga na TEP inaweza kuwa ni kwa sababu chama hiki tayari kilikuwa kimesajiliwa kikamilifu, na kilikuwa na miundombinu ya haraka kwa uchaguzi wa 2027. Kwa upande mwingine, Linda Mwananchi Movement, ingawa ilishinda kesi ya tribunal na kupata ruhusa ya kuhifadhi jina, bado ilikuwa na vizuizi vingi vya usajili na mashindano ya majina. Kwa hivyo badala ya kusubiri urasimu na hatari ya jina kufutwa tena, Sifuna alichagua gari lililo tayari — TEP.

 

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Sifuna alisisitiza kuwa TEP itakuwa chama cha wananchi, kitakachoweka raia katikati ya maamuzi, kusikiliza kabla ya kuamua, na kuwajibika kwa kila hatua. Aliahidi uongozi wa uwazi, usawa na mshikamano wa kitaifa, akisema chama hiki hakitakuwa cha mtu binafsi, bali cha wananchi wote waliotafuta mabadiliko.

 

Lakini hatua hii imeleta mkanganyiko kwa wafuasi wake. Wengi walitarajia Linda Mwananchi iwe alama ya upinzani mpya, sasa wakijiuliza kama itabaki kama harakati ya wananchi au itaunganishwa ndani ya TEP. Hatari ni kupoteza utambulisho wa harakati na kuchanganya wafuasi, lakini faida ni dhahiri, uhalali wa kisheria, miundombinu ya haraka na jukwaa thabiti kwa uchaguzi wa 2027.

 

Na sasa tunabaki tukijiuliza. je, uamuzi wa Sifuna kuingia TEP ulikuwa kweli kwa sababu ya urahisi wa kisheria na njia ya haraka au ni mkakati mkubwa zaidi unaoandaliwa nyuma ya pazia la siasa za upinzani?

Our Correspondent Avatar