Familia zilizopotelewa na ndugu zao watano katika mazingira ya kutatanisha maeneo ya Kariakoo ‘Kamata’ wameomba kuonana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi ili awasaidie, katika kuwapata ndugu zao.
Famili hizo zimesema zimeamua kufanya hivyo baada ya kuona hawapati msaada kutoka Jeshi la Polisi tangu walivyoripoti Desemba 27 bali wanaona wanazungushwa tu bila kujua nini kinaendelea.
Viajana hao walipotea mnamo Desemba 26, maeneo ya Kamata, Kariakoo jijini Dar es salaam na hadi sasa hawajaonekana wala hakuna taarifa zozote zinazowahusu iwapo wamekufa au wazima
Hata hivyo Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro akizungumza na wanahabari amesisitiza kuwa taarifa hizo ameshazipitia na kuagiza zifanyiwe kazi kama taarifa nyingine zinazofikishwa kituo cha polisi.
Kamanda Muliro amesema kuwa mfumo wa utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi, taarifa yoyote inapopatikana inafanyiwa kazi kwa sababu wakati mwingine taarifa zinazotolewa zinaweza kuwa za kweli au si za kweli.
“Taarifa ya kupotea vijana hao mimi ninayo nimetoa maagizo zifanyiwe kazi kama zilivyotaarifa zingine za kawaida zinazofikishwa kwenye vyombo vya dola ikiwemo Polisi,”amesema Kamanda Muliro
Ndugu wa vijana hao wamesema tangu kupotea kwa jamaa zao wamekuwa hawafanyi shughuli zao na wanakosa amani ya moyo kwa sababu hawajui ndugu zao huko waliko wako katika hali gani.
Wamebainisha kuwa hadi sasa wamezunguka Hospitali zote za Serikali hapa Dar es salaam pamoja na vituo vya Polisi bila mafanikio yoyote.
Waliopotea ni Tawfiq Mohamed, Self Swala, Edwin Kunambi, Hemed Abass na Rajabu Mdoe.Kwa mujibu wa familia zao siku ya mwisho mmoja wao alituma ujumbe mfupi wa simu ukieleza wamekamatwa maeneo hayo wakiwa kwenye gari IST nyeusi na wanapelekwa Kituo cha Polisi Central.
Vijana wao walikuwa wanajihusisha kuuza simu Kariakoo mtaa wa Aggrey walipotea wakiwa njiani kuelekea ufukweni Kigamboni kusherekea sikukuu ya krismas.