Dar yaongoza kwa wagonjwa wa corona

Visa hivyo vimeripotiwa katika kipindi cha Januari 29 hadi Februari 6, mwaka huu, huku wagonjwa wapya 76 kati ya 78 waliolazwa wakiwa ni wale ambao hawajachanjwa na vifo...

0

Mkoa wa Dar es Salaam umetajwa kuongoza kwa idadi kubwa zaidi ya waliothibitika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona ukiwa na wagonjwa wapya 184 kati ya visa vipya 252 vilivyoripotiwa.

Visa hivyo vimeripotiwa katika kipindi cha Januari 29 hadi Februari 6, mwaka huu, huku wagonjwa wapya 76 kati ya 78 waliolazwa wakiwa ni wale ambao hawajachanjwa na vifo vilikuwa vitatu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Aifello Sichalwe, visa hivyo vipya ni kati ya watu 8,529 waliopimwa katika kipindi hicho, sawa na asilimia tatu.

“Tangu ugonjwa huu ulivyoripotiwa kwa mara ya kwanza hapa nchini mnamo Machi 2020 hadi kufikia Februari 6, mwaka huu, jumla ya watu 33,482 walithibitika, sawa na asilimia 7.6 kati ya 442,566 waliopima na jumla ya watu 792 wamepoteza maisha,” alibainisha taarifa hiyo.

“Kwa siku ya Februari 6, mwaka huu, wagonjwa mahututi tisa waliripotiwa na wote walikuwa ambao hawajachanja chanjo ya UVIKO-19 na mgonjwa mmoja ameripotiwa kuwa kwenye mashine ya kusaidia kupumua na alikuwa hajachanjwa.”

Mganga Mkuu  alisema vifo vitatu vilivyotokea kwa kipindi hicho katika mikoa ya Dodoma, Morogoro na Manyara na vyote vilikuwa vya wagonjwa ambao hawajachanjwa.

Alisema serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo nchini ili kuwezesha wananchi kupata kinga dhidi ya ugonjwa huo ambapo hadi Februari 6, mwaka huu dozi 9,845,774 za chanjo zilikuwa zimepokewa nchini.

“Tangu kuanza kwa zoezi la uchanjaji nchini mpaka kufikia Februari 6, mwaka huu jumla ya watu 2,117,387, sawa na asilimia 3.67 wamepata dozi kamili ya chanjo,” alisema.

Aidha Mganga Mkuu aliwataka wananchi kuhakikisha wanapata dozi kamili za chanjo, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa kwa usahihi, kuzingatia usafi binafsi kwa kunawa mikono, kuwahi kwenye vituo vya afya wanapohisi dalili za ugonjwa huo na kuzingatia kufanya mazoezi.

In this article

East Africa Premier News Source with Top Stories, Special Features and more.
Uncensored & Undaunted