Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, nchini Tanzania itatoa uamuzi juu ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu Februari 18, ya iwapo wanakesi ya kujibu au la
Maamuzi hayo yamefikiwa leo baada ya Jopo la Mawakili wa upande wa Jamhuri kuiiambia Mahakama hiyo kuwa wamefunga ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani cha Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu kwa kuishia na shahidi wa 13
Upande huo wa mashtaka umefunga ushahidi huo ukidai ushahidi uliotolewa na mashahidi 13 kati ya 24 waliopanga kuwaita mahakamani hapo, unaonesha washtakiwa wote wanne wana kesi ya kujibu.
Akiwasilisha hoja hiyo mbele ya Jaji anayesikiliza kesi hiyo Jaji Joachim Tiganga, kwa niaba ya mawakili wenzake Wakili Mwandamizi wa Serikali Robert Kidando amesema
“Mheshimiwa Jaji Baada ya Shahidi huyu namba 13 Tumefanya Assessment Ya Kesi Yetu Kwa Maana ya Ushahidi Ambao Umetolewa Mpaka Sasa ni Maoni yetu Kwamba tume’ Discharge Burden ambayo tunatakiwa Kisheria hivyo tunaialika Mahakama Yako tukufu” amesema Wakili Kidando na kuongeza kuwa
“Chini ya Kifungu cha 41 (1) cha Sheria Ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Rushwa ya 2019,Uone Kwamba Washtakiwa Wote Wanne Wanayo kesi Ya Kujibu, Hivyo taratibu za Sheria zifuatwe ili Shauri hili liweze Kuendelea Katika Hatua zinazifuatia za Kuanza Kujitetea”
Baada ya kusikiliza hoja iliyoletwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kidando mahakama hiyo ikakubaliana na ombi la kufunga na inafunga kesi upande wa mashtaka kama ilivyoombwa mahakamani.
Hata hivyo Jaji Tiganga aliwauliza upande wa utetezi kuwa iwapo wana kitu cha kusema ndipo wakili anayeongoza jopo la mawakili wa utetezi Peter Kibatala akasimama na kuiomba mahakama iwaruhusu kufanya mawasilisho ya mdomo ya hakuna kesi ya kujibu huku akiiomba wapewe mwenendo wa kesi kuanzia mwanzo hadi upande wa mashtaka ulivyofunga.
Jaji Tiganga aliwaeleza mawakili wa utetezi kwamba tangu kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo karani wake amechapa kurasa 1400 za kesi hii, na huenda hadi kufikia jana na leo anaweza kuwa amechapisha karatasi zenye kurasa 1500.
Kufuatia majibu hayo mawakili wa pande zote mbili wakaomba nafasi kwa Jaji kwenda kujadiliana pembeni kisha warudi katika chumba cha mahakama.
Mara baada ya muda kupita, Mahakama ikarejea ambapo jaji Tiganga amesema kuwa baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili na makubaliano ya mawakili wa pande zote atatoa uamuzi wa iwapo Mbowe na wenzake wanakesi ya kujibu au la.
Kesi hii ilianza kusikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu Uchumi na Rushwa Septemba 3, 2021, ambapo upande wa Jamhuri walisema watakuwa na mashahidi 24 na vielezo 19.
Shahidi wa leo Inspekta Tuamaini Swila ndiye aliyefunga pazia la mashahidi wa Jamhuri na ni miongoni mwa mashahidi 13 wa Jamhuri, waliofika mahakamani hapo kati ya 24 waliopangwa kuitwa.
Mashahidi wengine wa Jamhuri waliowahi kufika kutoa ushahidi katika kesi hiyo ni Luteni Denis Urio, Justine Kaaya, aliyekuwa msaidizi wa Lengai Ole Sabaya, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro. Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, ACP Ramadhan Kingai. Inspekta Mahita Omary Mahita.
Mrakibu wa Polisi, Jumanne Malangahe, Inspekta Goodluck Minja na Inspekta Innlcent Ndowo.