Ikiwa leo ni siku ya wanawake duniani ambayo kauli mbiu kwa mwaka huu ni “usawa wa kijinsia leo kwa ajili ya maendeleo endelevu kesho”, lakini je wajua chimbuko la siku hii lilianzia wapi?
Siku ya wanawake duniani hujulikana pia kama IWD kwa ufupi, ilikua inatokana na vuguvugu la wafanyakazi na kuwa tukio la kila mwaka linalotambuliwa na Umoja wa Mataifa (UN).
Chimbuko lake lilianzia mwaka 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika Jiji la New York wakidai muda mfupi wa kufanya kazi, malipo bora na haki ya kupiga kura.
Mwaka mmoja baadaye, ambao ni 1909 mwanamke aliyejulikana kwa jina la Clara Zetkin alipendekeza kuanzishwa kwa siku ya wanawake duniani katika mkutano wa wafanyakazi wanawake uliofanyika katika jiji la Copenhagen nchini Denmark.
Clara Zetkin alikua ni mwanaharakati wa kikomunisti na mtetezi wa haki za wanawake. Alipendekeza wazo hilo ikiwa ni sehemu ya kuwatetea wanawake duniani kote.
Kwenye mkutano huo kulikuwa na wanawake 100, kutoka nchi 17, na walikubali pendekezo lake kwa kauli moja.
Siku hii Iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mnamo 1911, huko Austria, Denmark, Ujerumani na Uswizi. Miaka 100 iliadhimishwa mwaka 2011, kwa hivyo mwaka huu tunasherehekea Kitaalam Siku ya 111 ya Kimataifa ya Wanawake.
Siku ya Wanawake Duniania iliidhinishwa rasmi mwaka 1975 wakati Umoja wa Mataifa ulipoanza kuadhimisha siku hiyo. Mada ya kwanza iliyopitishwa na UN (mwaka 1996) ilikuwa “Kuadhimisha Yaliyopita, Mipango ya Siku zijazo”.
Siku ya Kimataifa ya Wanawake imekuwa siku ya kusherehekea jinsi wanawake walivyofikia katika jamii, katika siasa na uchumi, huku mizizi ya kisiasa ya siku hiyo ikimaanisha migomo na maandamano inaandaliwa ili kuongeza uelewa wa kutokuwepo usawa.